MUUGUZI AFARIKI CHOONI KWENYE JENGO ALIKOENDA KUPATA USHAURI MATATIZO YA NDOA

Polisi katika kaunti ya Embu nchini Kenya wameanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha kutatanisha cha muuguzi wa kike mwenye umri wa miaka 28.

KBC iliripoti kuwa muuguzi huyo alipatikana akiwa amefariki ndani ya choo cha jumba moja katika kaunti ya Embu.

Mwanamke huyo anayefanya kazi katika Kituo cha Afya cha Kiritiri alikuwa ameenda kutafuta ushauri kuhusu matatizo katika ndoa yake.

Mwili wake baadaye uligunduliwa ukiwa umelala sakafuni, katika kile ambacho polisi wanashuku kuwa huenda alijitoa uhai.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mwanamke huyo alijifungia ndani ya choo kabla ya kumeza dawa za kutuliza maumivu kupita kiasi. 

Mtaalamu wake Liza Gota alisema muuguzi huyo alikuwa mteja wake na alikuwa anakuja kwa kikao cha ushauri kwa kuwa alikuwa na matatizo ya ndoa.

"Amekuwa akitumia vibaya dawa ya matibabu, dawa ya kutuliza maumivu yenye nguvu sana, na baada ya muda, aliizoea kwa kuwa alikuwa na tatizo la mgongo mbali na masuala ya ndoa," mshauri huyo alisema.

Alikuwa anatoka Bonde la Ufa lakini aliolewa na mwanaume kutoka kaunti ya Embu ambaye pia ni daktari.

Maafisa wa polisi waliusafirisha mwili wake hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Embu Level 5 huku familia na marafiki wakisubiri matokeo ya uchunguzi wa maiti.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post