SERIKALI YAPONGEZA KASI YA WANANCHI WA NGORONGORO KUHAMA KWA HIARI.


Na John Mapepele

Serikali imelipongeza wimbi kubwa la wananchi wanaopisha kwa hiari zoezi la uhifadhi kwenye Hifadhi ya Ngorongoro na kuhamia maeneo mengine.

Kauli hiyo imetolewa leo Februari 1, 2024 na Kamishina wa Uhifadhi wa Ngorongoro, Richard Kiiza wakati akiliaga kundi la takribani wananchi 600 walioanza safari majira ya saa 12:30 asubuhi kutoka ofisi ya zamani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuelekea Msomera.

"Ndugu zangu nawashukuru kwa hamasa kubwa mliyonayo Sasa ya kuanza kuondoka kwa hiari hifadhini kupisha uhifadhi maana sasa spidi ya kujiandikisha imekuwa kubwa katika kipindi kifupi" amefafanua Kamishina Kiiza.

Amewahakikishia kuwa dhamira ya Serikali ni njema ya kutaka kuboresha maisha yao na kuwaomba wawndelee kuwashawishi wenzao waliobaki ili pia waboreshe maisha yao.

Mwakilishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, John Mapepele ambaye pia ndiye Msemaji wa Wizara hiyo anasisitiza" Nimefarijika kuona wananchi wanaofurahia maisha wakifika Msomera wamekuwa mabalozi wazuri wa kuwaelezea jinsi Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ilivyoboresha maisha yao"

Hadi sasa kundi hili linakuwa kundi la tano kwenda eneo la Msomera ikiwa ni jumla ya kaya 934 zenye jumla ya watu 5747 na mifugo 26227.

Serikali imekuwa ikizingatia haki zote za msingi wakati wa kuwahamisha wananchi wanaopisha uhifadhi kwa hiari ikiwa ni pamoja na kujengewa nyumba bure, kulipwa fidia ya maendelezo, kupewa shamba la ekari tano, kifuta jasho cha milioni kumi, kusafirishwa wao na mizigo yao na kuendelea kupatiwa mahindi kwa ajili ya chakula kwa mwaka mmoja na nusu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post