MAADHIMISHO MIAKA 47 YA CCM...MBUNGE CHEREHANI ATOA MADAWATI 975 YA MIL 63.3


Na Mathias Canal, Ushetu-Kahama

Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe Emmanuel Cherehani kupitia Ofisi ya mbunge ametoa madawati 975 yenye thamani ya Shilingi 63,375,000 ili kuimarisha sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na mazingira mazuri ya kujifunzia katika Jimbo la Ushetu.

Amesema kuwa sekta ya elimu ni muhimili mkuu katika kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja, kaya na Taifa kwa ujumla wake hivyo kuna kila sababu ya wadau na wananchi kujitokeza kuchangia katika maeneo mbalimbali.

Mbunge Cherehani ameyasema hayo tarehe 3 Februari 2024 wakati wa maadhimisho ya miaka 47 ya Chama Cha Mapinduzi yaliyofanyika Katika kijiji na Kata ya Igwamanoni Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe Christine Mndeme amempongeza Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe Emmanuel Cherehani huku akisema amekuwa kiongozi mwenye kutafuta suluhu ya matatizo ya wananchi sio aina ya viongozi walalamishi.

Mndeme amewasihi wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Amemuagiza kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga kuondoa kero ya kukamata wananchi wanaobambikiziwa kesi badala yake kushughulika na madalali wanaowabambikizia kesi wananchi wenzao wasiojiweza.

"Na Katika hili nakuagiza RPC kamata madalali wote wanaobambikizia kesi wananchi kwani wanalipaka matope jeshi la polisi hali kadhalika wanakipaka matope Chama Cha Mapinduzi" Amesisitiza RC Mndeme

Kuhusu mafanikio yaliyofanywa na serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amesema zaidi ya Trilioni 4 zimetolewa na serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa wa Shinyanga ikiwemo sekta ya elimu, afya, maji, miundombinu, kilimo, Uwekezaji, Nishati, N.k

Katika Wilaya ya Kahama Maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa CCM yameandaliwa na Umoja wa Wanawake na kuchagizwa na kauli mbiu isemayo "Miaka 47 ya CCM, Shiriki Uchaguzi kwa uadilifu na Kazi Iendelee".

Awali akitoa taarifa ya Maadhimisho hayo mbele ya mgeni rasmi, Katibu wa UWT wilaya ya Kahama Bi Happiness Mpenah ameeleza kuwa hali ya kisiasa katika wilaya hiyo inaendelea kuimarika huku akieleza kuwa wanawake wana imani kubwa na serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan.

Pia UWT imempongeza Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe Emmanuel Cherehani kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutatua changamoto mbalimbali za wananchi kwa kuwa mstari wa mbele kwenye masuala mbalimbali yanayohusu wanawake.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post