DKT HUSSEIN :ACHENI KUTUMIA MITISHAMBA KUTIBU MACHO





Daktari Bingwa wa Macho katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo Dkt Hussein Abbas Tayebji amewataka wananchi wanaotumia njia ya kienyeji kutibu macho ikiwemo kutumia mkojo na maji ya chumvi kuweka kwenye macho kama tiba kuacha kufanya hivyo kwani wanaweza kupata madhara makubwa zaidi.

Kauli ya Daktari hiyo imekuja siku chache baada ya kuwepo kwa wimbi la Ugonjwa wa Macho maarufu kama Red Eyes likiendelea kuwatesa watanzania katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Dkt Hussein ambaye pia ni Mratibu wa Macho Mkoa wa Tanga aliyasema hayo leo wakati akizungumzia kuhusu ugonjwa huo kwa mkoa ambapo alisema mpaka sasa zaidi ya wagonjwa 90 wameugua huku asilimia kubwa wakitokea kwenye Jiji la Tanga

Alisema kwamba badala yake wananchi wanapougua ugonjwa huo wafike kwenye Vituo vya Afya au Hospitali kwa ajili ya kuwaona madaktari ili kuweza kupatiwa matibabu ikiwemo kupewa ushauri nini wafanye.

“Lakini niwaambie kwamba watu waache kutumia mitishamba,kuweka mkojo kwenye macho na maji ya chumvi kwani kufanya hivyo kunaweza kunaweza kusababishia matatizo makubwa sana huku akishauri wafike kwa daktari ili waweze kupata tiba sahihi”Alisema

Aidha Daktari huyo aliwataka pia wale wanaopata maambukizi ya ugonjwa huo wasitumie dawa za mwenzake maana wakitumia dawa vibaya wanaweza kupata matatizo makubwa kwani kila mtu anakuwa na kipimo chake cha matumizi.

Dkt Hussein alisema kwamba mtu mmoja akipata ugonjwa huo anaweza kumuambukiza mwenzake huku akitoa tahadhari wananchi waache kushirikiana kwenye vitu kama vile Taulo,Vitambaa(leso) ya mwenzake ikiwemo maji ya choo.

Hata hivyo Dkt Hussein pia alisema kwamba hivi sasa wanaendelea kutoa elimu kwa wanafunzi ikiwemo maeneo mbalimbali ili kuweza kujikinga na ugonjwa huo na hatua za kukabiliana nazo wanapokumbana na hali hiyo.

"Lakini mtu akiumwa na ugonjwa huo ikiwemo wanafunzi,watumishi wanashauriwa kupumzika nyumbani angalau siku mbili tatu ili asiendelee kusambaza kwa watu wengine "Alisema Dkt Hussein

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post