WAFANYABIASHARA WADOGO, MAKUNDI MAALUM YAPEWE KIPAUMBELE UNUNUZI WA UMMA - DKT. BITEKO


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
akishuhudia utiaji saini hati ya makubaliano kati ya Mamlaka ya
Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) inayolenga kuwawezesha wafanyabiashara wadogo, wa kati na makundi maalum katika ununuzi wa umma, jijini Dodoma tarehe 07 Februari, 2024.


· Ashuhudia makubaliano ya PPRA na NEEC kuwezesha Makundi Maalum
· Aagiza rufaa za makundi maalum PPRA zisikilizwe haraka
· Ataka makundi maalum yajengewe uwezo kuweza kushindana.


Na Mwandishi Maalum. Dodoma


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko ameiagiza Taasisi zote za ununuzi nchini (Serikali na Binafsi) kuhakikisha zinatoa kipaumbele katika manunuzi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa ndani ya nchi ili kukuza uchumi wa Watanzania na wazingatie kutoa kipaumbele kwa wafanyabiashara wadogo na makundi maalum.



Amesema hayo tarehe 07 Februari, 2024 Jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini hati ya makubaliano kati ya Mamlaka ya Udhibiti wa
 Ununuzi wa Umma (PPRA) na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ili kujenga ushirikiano unaolenga kuchochea ushiriki wa Wafanyabishara Wadogo, wa kati na Makundi Maalum katika masuala ya ununuzi wa umma.

“ Kusainiwa kwa hati hii leo, kunazidi kuboresha mazingira ya
Watanzania kushiriki kwenye uchumi wa nchi yao, hasa watu kutoka
makundi maalum. Na haya ni maelekezo ya Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha watanzania wote wanashiriki kwenye shughuli za kiuchumi, hivyo NEEC, PPRA, Taasisi nyingine za Serikali na Binafsi wawezesheni watanzania kushika uchumi wa nchi na muone fahari katika hili.”Amesema Dkt. Biteko



Kupitia hafla hiyo Dkt. Biteko ameitaka PPRA kuzidi kuboresha huduma zake kwa Watanzania ikiwa ni Pamoja na kuharakisha mchakato wa rufaa zinazowasilishwa kwenye mamlaka hiyo hususani zile zinazohusisha waombaji wa zabuni kutoka makundi maalum ili kuchochea kasi ya ukuaji wa Uchumi wa mtu mmoja mmoja na hatimaye Uchumi wa Taifa. 

Amezitaka mamlaka hizo kujikita zaidi katika uwezeshaji wa wananchi kwa kutoa elimu badala ya kubaki kuwa wadhibiti pekee.

Ameziagiza NEEC na PPRA kufanya tathmini na kutoa tuzo kwa watoa huduma wanaofanya vizuri katika uwezeshaji wa makundi maalum suala litakalochagiza ushindani miongoni mwa watoa huduma na hatmaye kukuza Uchumi.

Amesema makubaliano hayo yatatumika kama jukwaa la kuwahamasisha watu wa kundi hilo kushiriki na kuimarisha Uchumi wa mtu mmoja mmoja, kuimarisha wigo wa walipakodi na hivyo kukuza Uchumi wa nchi.

Ameipongeza PPRA kwa kuweka kanuni ya ushirikishaji makundi maalum kwenye manunuzi ambayo imeelekeza kuwa asilimia 30 ya zabuni zotezitolewe kwa washiriki kutoka makundi maalum ambao ni wanawake,vijana, Wazee na wenye mahitaji maalum.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama, amesema kusainiwa kwa hati ya makubaliano kati ya PPRA na NEEC ni ushahidi wa namna Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoamua kwa dhati kushikirisha makundi ya watu maalum kwenye uchumi na ujenzi wa Taifa.

Amesema kuwa, makubalinao hayo yataongeza ushiriki wa makundi maalum kwenyenunuzi ya umma na hii itaongeza uwezo wa watanzania katika uzalishaji malighafi na bidhaa pamoja na utoaji wa huduma ndani ya nchi.

Amesema kuwa, katika suala hilo la watanzania kushiriki katika kukuza uchumi wa Taifa, Ofisi anayoisimamia itaendelea kuisimamia NEEC ili iendeelee kuratibu utekelezaji wa sheria na hasa zile zinazohusu ushiriki wa watanzania kwenye miradi mbalimbali na kujenga uchumi wa nchi.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa, kusainiwa kwa hati hiyo kutaondoa mapungufu yaliyokuwa yakijitokeza kwenye masuala ya ununuzi wa umma hasa kwa watu wenye makundi maalum hivyo baada ya kusainiwa kwa hati hiyo utekelezaji wake utaanza mara moja.

Amesema siku zote Serikali inalenga katika kuwawezesha wananchi kiuchumi hali itakayoongeza walipakodi na hasa kwa watu wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi na wenye uwezo badala ya wananchi wa hali ya chini.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, Baadhi ya Naibu mawaziri, Makatibu Wakuu wakiongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri wa Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonaz, baadhi ya Wabunge na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post