RASIMU YA TAARIFA YA TATHMINI YA USHIRIKI WA WATANZANIA KATIKA MIRADI YA KIMKAKATI NCHINI KUJADILIWA


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Anderson Mutatembwa akifungua kikao kazi cha wataalam cha kujadili Rasimu ya Taarifa ya Tathmini ya Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati Uwekezaji inayotekelezwa nchini kilichofanyika Mkoani Singida, tarehe 29 Januari, 2024.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Anderson Mutatembwa (Kulia) na Mkurugenzi Uwezeshaji Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi, Kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Condrad Millinga wakifuatilia jambo, katika kikao kazi cha wataalam cha kujadili Rasimu ya Taarifa ya Tathmini ya Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati Uwekezaji inayotekelezwa nchini kilichofanyika Mkoani Singida, tarehe 29 Januari, 2024.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uboreshaji wa Mifumo ya Masoko nchini Bw. Charles Ogutu akizungumza wakati wa kikao kazi cha wataalam cha kujadili Rasimu ya Taarifa ya Tathmini ya Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati Uwekezaji inayotekelezwa nchini kilichofanyika Mkoani Singida.

Baadhi ya Watalaam katika kikao kazi cha kujadili Rasimu ya Taarifa ya Tathmini ya Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati Uwekezaji inayotekelezwa nchini kilichofanyika Mkoani Singida.

(HABARI NA PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

NA; MWANDISHI WETU – SINGIDA
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Anderson Mutatembwa, ameongoza kikao kazi cha wataalam kujadili Rasimu ya Taarifa ya Tathmini ya Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati Uwekezaji inayotekelezwa nchini kilichofanyika Mkoani Singida Tarehe 29 Januari, 2024.

Bw. Mutatembwa, alisema dhana ya Ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati yaani (Local content) ni dhana inayolenga katika kuhakikisha kuwa thamani ya ziada inayopatikana kwenye uchumi kutokana na utekelezaji wa miradi ya kimkakati na uwekezaji inabaki nchini na kuchangia ukuaji wa uchumi pamoja na kunufaisha Watanzania na Taifa kwa ujumla.

Aliendelea kusema kuwa, Serikali inatekeleza dhana hii kwa kuhakikisha ajira kwa watanzania zinapatikana, uanzishwaji wa kampuni za ubia, matumizi ya malighafi zinazopatikana nchini katika uzalishaji na utoaji wa huduma, manunuzi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa au zinazotolewa na kampuni za Kitanzania na uhawilishaji wa teknolojia.

Aidha aliongeza kusema kuwa, dhana hiyo inahakikisha uwepo wa ushiriki wa kampuni za kitanzania, na ushirikishwaji wa jamii zinazoishi katika maeneo ya uwekezaji au miradi inapotekelezwa.

Akiongea na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa kikao kazi hicho, Mkurugenzi Uwezeshaji Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi, Kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Condrad Millinga alisema moja ya eneo linalofanyiwa kazi katika kikao kazi hiki ni kuona watanzania watashiriki vipi hasa katika eneo la ajira za ndani kwa kuwajengea uwezo waweze kushiriki kwa maana ya wenye ujuzi na wasiokuwa na ujuzi, aidha kuangalia eneo la matumizi ya malighafi na rasilimali zilizopo nchini katika miradi mikubwa.
“Tunauzalishaji unaotumika lakini kwa kiwango kidogo sana kulinganisha na mahitaji halisi, kumbe tunahitaji wenyewe kujipanga ndani lakini pia kushirikiana na wenzetu wanaotoka nje ili kuzalisha kulingana na mahitaji katika maeneo ya Uwekezaji,” Alisisitiza

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uboreshaji wa Mifumo ya masoko Nchini Bw. Charles Ogutu alisema mapitio ya rasimu hiyo yatahakikisha kwamba wanatanzania wanashirki kikamilifu na kunufaika na miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa nchini.

“Bila kusahau kwamba hakuna mradi mkubwa ambao hautegemei kilimo kwa hiyo tunakitazama kilimo kama ndiyo sekta mama inayobeba sekta zote kwa hiyo ni vizuri sana mazingira ya kibiashara na mazingira yote katika sekta ya uwekezaji zijumuishe sekta ya Kilimo.” Alibainisha

Akiongea katika kikao kazi hicho kilichohusisha wataalam kutoka Serikali kuu,Taasisi, MDA’s na sekta binafsi mtaalam wa uwekezaji wa Kimataifa (FDI) na Uchumi mkubwa Dkt. Juma Makaranga alisema ni muhimu kwa makampuni ya ndani kufanya biashara na makampuni makubwa ya nje kwa kusaidiwa kutengenezwa na kuwainua kiteknolojia, usimamizi na kitaaluma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments