MBUNGE LUGANGIRA ATAKA MATUMIZI YA MITANDAO KATIKA UCHAGUZI YAINGIE KATIKA SHERIA
MBUNGE wa Viti Maalumu, Neema Lugangira ameshauri Mswada wa Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi uwe na Ibara inayoongelea masuala ya Matumizi ya Mitandao katika Uchaguzi ikiwemo (Akili Mnemba - AI).

Lugangira ametoa ushauri huo leo jijini Dar es Salaam wakati akichangia kwenye mkutano maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa unaoshirikisha wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kujadili miswada ya sheria za uchaguzi na mswada wa sheria za vyama vya siasa.

Alisema Novemba 2023, Jumuiya ya Tume za Uchaguzi Afrika (Association of African Election Authorities) ilipitisha Mwongozo wa Matumizi ya Mitandao katika Uchaguzi barani Afrika na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania ni Mjumbe katika Jumuiya hiyo, hivyo itakuwa sio jambo jema kutunga Sheria ambayo inakinzana na maazimio hayo.

"Mswaada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi haijagusia kabisa suala la Matumizi katika Uchaguzi, jambo ambalo limeshathibika kuwa moja ya maeneo yenye changamoto kubwa katika chaguzi zetu," alisema

Alisema ni lazima kuangalia pia athari za teknolojia mpya kama akili mnemba “artificial intelligence” katika Uchaguzi kwa kuwa tayari dunia imekwenda huko.

"Napenda kushauri na kusisitiza Sheria hii ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi uhakikishe inaongezwa Ibara Mpya katika eneo hili la Matumizi ya Mitandao katika uchaguzi sababu Jumuiya ya Tume za Uchaguzi Afrika ambapo Tume yetu ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania ni Mjumbe, alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post