Na Mwandishi wetu ETE
Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Sanamare Tanzania ikishirikiana na wakazi wa Kibugumo, Kata ya Mjimwema Kigamboni, Taasisi mbalimbali za Mazingira na vyuo mbalimbali pamoja na wananchi kwa pamoja wamefanya usafi ndani ya mikoko eneo la Kibugumo sehemu ambayo imekuwa korofi kutokana na kukithiri kwa kutupwa taka kutoka majumbani bila utaratibu jambo ambalo limesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira hayo ya Mikoko, zoezi hilo lilienda sambamba na upandaji wa Mikoko katika eneo ambalo lilikuwa na uhitaji wa kufanya hivyo.
Akizungumza baada ya zoezi la usafi na upandaji miti Pius Mollel kutoka taasisi ya Sanamare Tanzania ambao ndio waandaji wa zoezi hilo alisema anashukuru kwa wadau wote na wananchi kwa ujumla wanaopenda mazingira kwa kujitokeza kwa ajili ya kufanya usafi na kupanda Mikoko amesema ni muhimu kuendelea kufanya hivyo kwa sababu jukumu la mazingira ni la kila mtu.
Kwa upande wake Dkt. Kulindwa ambaye ni Mkufunzi wa Chuo cha Ushirika Moshi alisema kuwa muungano wa watu wote bila kujali umri katika kutunza mazingira ni muhimu kuendelea kuyatunza na kuongeza kuwa taasisi mbalimbali ziendelee kufanya utafiti zaidi kuhusu maeneo kama ya mikoko ili kuendelea kupambana na mabadiliko ya Tabianchi.
Naye Mwenyekiti wa BMU Kata ya mji mwema , Abdul Mweta aliwashukuru wadau wote walioweza kushiriki zoezi la usafi na kuwaomba waendelee na umoja huo huo sio katika kata ya mjimwema tu bali na maeneo mbalimbali ili kuyanusuru Mazingira.
Wadau mbalimbali wa Mazingira wakizungumza kwa nyakati tofauti walitoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea na juhudi za kuendelea kuweka mazingira sawa kwa ajili ya sasa na vizazi vijavyo
Wakati huo huo ETE walishiriki katika kufanya usafi eneo hilo kwa lengo la kuweka mazingira safi lakini pia kutumia Dijitali kuyasemea mazingira ambayo hayawezi kujisemea yenyewe, kwa Hashtag #ETEMazingiraKidijidali kwa kutumia mitandao ya kijamii na majukwaa mbalimbali ya mtandaoni.
Picha zote na Fredy Njeje - Mdau wa Mazingira