Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa mkoani hapa imemtunuku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan tuzo ya heshima ya kutunza na kulinda urithi wa historia ya wapigania uhuru wa Nchi za kusini mwa Afrika na kuchochea utalii nchini.
Nchi hizo ni pamoja na Zimbabwe, Angola, Afrika Kusini, Namibia na Msumbiji ambazo Ziliweka kambi wilayani hapo wakati wa harakati za kutafuta uhuru wa nchi za Afrika ambapo Watanzania Walishiriki katika kutoa msaada kwa nchi hizo.
Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki wakati wa mbio za marathon zilizopewa jina la Kongwa African Liberation Marathon zilizobeba kauli mbiu ‘Kongwa mbeleko ya ukombozi wa Afrika’.
Akikabidhi tuzo hiyo kwa mgeni rasmi ambaye alikuwa mkuu wa wilaya ya Chemba Gerald Mongela ,Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Remidius Mwema amesema lengo ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kutangaza vivutio vya utalii na kulinda urithi wa taifa.
Awali akizungumza wakati wa mkutano Mongela amesema wilaya ya Kongwa ni miongoni mwa maeneo yenye mandhari nzuri inayofaa kwa uwekezaji utakaochochea utalii kutokana na kwamba eneo hilo ni kitovu cha Mkoa wa Dodoma.
“Tuendelee kuitunza historia ya Tanzania kwani moja ya ajenda ya Rais Samia amekuwa akisisitiza kuhakikisha jamii inatambua historia ya nchi yao ili kuwa katika nafasi nzuri ya kulinda na kuiendeleza, ndani ya historia hii kuna mila, desturi, lugha, urithi, uwajibikaji na uzalendo hii i fursa nzuri kwa Watanzania na Afrika kwa ujumla kutambua na kuendelea kujivunia mchango wa taifa la Tanzania katika ukombozi wa Afrika,” amesema
Aidha ameelekeza mbio hizo kuwa endelevu kila mwaka na kwamba maandalizi ya mwakani balozi za nchi zilizotumia eneo la Kongwa kupata mafunzo ya kijeshi zihusishwe kwenye maandalizi ili kuwezesha washiriki kutoka kwenye mataifa yao na hivyo kuzifanya mbio za kongwa marathon kuwa za kimataifa.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kongwa Remidius Mwema amesema Serikali kupitia Ofisi yake ina mpango wa kuboresha miundombinu katika maeneo ya kihistoria wilayani hapo ili kuwa moja ya sehemu zitakazovutia watalii lengo ni kutangaza utalii na historia ya ukombozi wa nchi za kusini mwa afrika.
Mwema ameeleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuenzi maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kutambua mchango wa Tanzania katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Afika na kwamba maeneo yote yaliyotumiwa na wapigania Uhuru yatabaki kuwa kumbukumbu ya kipekee.
Mkuu huyo wa wilaya ya Kongwa amezitaja nchi hizo ambazo viongozi wake waliweka kambi wilayani hapo kuwa ni takribani nchi tano ambazo ni Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe, Msumbiji na Angola.
"Ni muhimu Sehemu ya fedha zitazopatikana kwenye mbio hizo kusaidia kuboresha maeneo ya kihistoria yanayo patikana wilayani hapa hususani maswala ya kielimu hasa ukarabati wa madarasa yaliyotumiwa na madawati, " amesema
Naye,Msimamizi na mratibu wa Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika Boniface Kadili amesema kuwa Kongwa inakwenda kuingizwa kuwa kituo cha urithi wa taifa na baadaye kwenye urithi wa dunia kwani ina vigezo vyote.
Amesema hatua hiyo ni muendelezo wa program ya urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika wenye lengo la kutambua na kuhifadhi kumbukumbu za harakati za kutafuta uhuru wa nchi za Afrika ambapo nchi ya Tanzania ilishiriki katika kutoa msaada kwa nchi hizo.
Amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara kupitia kituo cha urithi imetenga fedha maalum kwa ajili ya kufanya ukarabati wa mahandaki yaliyotumiwa na viongozi wa nchi za kusini mwa Afrika ikiwemo handaki la Kongwa ambalo lilitumiwa na hayati Samora Machel akiwa kongwa kwa ajili ya kujihami na hatari.
"Nitumie fursa hii kuelekeza kuwa maadhimisho ya siku ya Afrika ambayo hufanyika Mei 25, kila mwaka, yafanyike hapa Kongwa kitaifa ili kuendelea kuitangaza eneo hili na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu utaliii uliopo Kongwa, " amesema
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, White Zuberi ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa tangu mwaka 2010 wamekuwa wakipambana ili kufanya Kongwa ipate hadhi inayostahili.
Amesema mara kaadha amekuwa akipokea ugeni kutoka nchi mbalimbali za Afrika ambao wanakuja kwa lengo la kuona makaburi ya mashujaa wao wa ukombozi lakini bado hawaoni umuhimu wa kuyahifadhi na kuyatunza kwa ajili ya kuyaenzi kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
“Mwaka 1995 kikosi cha Jeshi kiliondolewa Kongwa baada ya wapiganaji kuondoka lakini tunashukuru sasa Rais Samia Suluhu Hassan amerudisha kambi ya Jeshi kwenye eneo la kihistoria,” amesemamafunzo
Wilaya ya Kongwa ni moja ya maeneo yaliyotumiwa na wapigania uhuru wa Bara la Afrika ambapo yanapatikana makaburi ya wapigania uhuru waliopoteza maisha wakati wa vita vya ukombozi pamoja na handaki la kijeshi lililotumiwa na Rais wa Msumbiji Samora Machel kwa ajili ya kujificha .