POLISI SHINYANGA WAJIWEKA TAYARI KUKABILIANA NA UHALIFU KUELEKEA CHRISMAS NA MWAKA MPYA... BUNDUKI YAKUTWA SHULENI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akionesha silaha aina ya Pistol Browning ikiwa na risasi 12 ambayo ilitelekezwa au kusahauliwa na mmiliki wake katika  moja ya shule ya Mjini Shinyanga kutokana na uzembe katika kumiliki silaha hiyo.

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Kuelekea kipindi cha Sikukuu za Krismas na Mwaka mpya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limeendelea kujiweka katika hali ya utayari ili kukabiliana na vitendo mbalimbali vya kihalifu, na kuhakisha ulinzi na Usalama wa raia na mali zao unaendelea kuimarika.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumatano Novemba 29,2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amesema  Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limeendelea kufanya doria na misako katika maeneo yote ya Mkoa wa Shinyanga, kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi ambapo hadi sasa kuna jumla ya vikundi hai 209 vinavyoshirikiana na Jeshi la Polisi. 


"Pia tunaendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara katika msimu huu wa sikukuu ili kuimarisha usalama barabarani, na kuwapeleka mahakamani wale wote wanaovunja sheria za usalama barabarani",amesema.

 Amefafanua kuwa, kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita, jumia ya madereva 06 wa magari walipelekwa mahakamani kwa makosa ya usalama barabarani, madereva 6,499 wa vyombo vya moto walitozwa fine na pia madereva 03 walifungiwa leseni zao. 

Hata hivyo amesema, kwa kipindi hicho cha mwezi mmoja uliopita, hakukuwa na ajali mbaya iliyojitokeza katika mkoa wa Shinyanga.


 "Kwa upande wa mahakama, jumla ya kesi 19 ziliweza kufanikiwa ambapo kesi 03 za makosa ya kubaka zilihukumiwa kifungo cha kati ya miaka 30 hadi kifungo cha maisha, kesi 01 ya kulawiti ilihukumiwa kifungo cha maisha jela, kesi 01 ya shambulio la aibu ilihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na fidia ya shilingi millioni moja, kesi 03 za wizi zilihukumiwa kifungo cha mwaka 01 jela, kesi 01 ya ukatili dhidi ya mtoto ilihukumiwa kifungo cha miaka 03 jela pamoja na fine ya shilingi laki tano, pia kesi 01 ya kumtorosha mwanafunz ilihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela",ameeleza Kamanda Magomi.

"Vilevile kesi 01 ya kughushi nyaraka ilihukumiwa kifungo cha miaka 05 jela, kesi 01 ya wizi wa mtoto ilihukumiwa kifungo cha miaka 03 jela, kesi 02 za wizi wa mifugo zlihukumiwa kifungo cha mwaka 01hadi 05 jela na pia kesi 02 za kujeruhi zilihukumiwa kifungo cha mwaka 01 hadi 05 jela. Kesi zingine 02 za wizi wa Pikipiki ziliyohukumiwa kifungo cha miaka 02 na nyingine ya wizi ilihukumiwa kifungo cha miezi 06 jela na kulipa fidia ya shilingi milioni nane na kesi 01 ya kupatikana na bangi ilihukumiwa miaka 02 jela",ameongeza.

Ameongeza kuwa, katika mafanikio ya misako na doria wamefanikiwa kukamata jumla ya gramu 2205 pamoja na kete 61 za dawa za kulevya aina ya bangi, Pikipiki 11, mifuko 24 ya Cement, Ndoo 04 na makopo 04 ya rangi za majumba, Gypsum Powder na vifaa mbalimbali vya ramli chonganishi. 

Aidha kutokana na ushirikiano mwema kati ya Polisi na Jamii, amesema wananchi waliweza kutoa taarifa ya uwepo wa silaha aina ya Pistol Browning ikiwa na risasi 12 ambayo ilitelekezwa au kusahauliwa na mmiliki wake katika moja ya shule mjini Shinyanga kutokana na uzembe katika kumiliki silaha hiyo. 

Amesema jumla ya watuhumiwa 29 walikamatwa huku baadhi yao wakifikishwa mahakamani na wengine kupewa dhamana wakisubiri upelelezi wa kesi zao kukamilika.

 "Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linatoa wito kwa wananchi wake kufuata Sheria na kutojihusisha na vitendo vya kiuhalifu, Madereva na watumia barabara kufuata sheria za Usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima, na litaendelea kuchukua hatua kali za Kisheria kwa yeyote atakayejihusisha na vitendo vya uhalifu",amesema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post