Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe akizungumza
Afisa mtendaji mkuu wa Wakala wa Vipimo Stella Kahwa
Na Mariam Kagenda - Kagera
Serikali itahakikisha wananchi wanaendelea kutumia vipimo sahihi kwa wakati wote katika sekta zote hasa katika sekta ya kilimo.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe amesema hayo baada ya kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara,Kilimo na Mifugo kufanya ziara mkoani Kagera na kuzungumza na Taasisi ya Wakala wa Vipimo.
Mhe. Kigahe amesema kuwa yapo maeneo yanayolalamikiwa katika suala la vipimo ikiwa ni pamoja na sekta ya kilimo kwani vipimo katika mazao ya kilimo bado ni changamoto ambapo wafanyabiashara wengi bado hawajawa tayari kufuata taratibu za kununua mazao kwa vipimo.
Ameongeza kuwa kama Wizara moja ya sheria inayosimamiwa na Wakala wa Vipimo inalazimisha kila mmoja awe mnunuzi au muuzaji kutumia vipimo hivyo watahakikisha mazao yote yanauzwa kwa vipimo.
Amesema kuwa tayari kuna kamati maalum ambayo imeshaundwa kutathimini changamoto iliyopo ili kuhakikisha wanakomesha kuuza bidhaa au mazao kwa rumbesa na kamati hiyo itakuja na mkakati maalum.
Kwa upande wake Afisa mtendaji mkuu wa Wakala wa Vipimo Stella Kahwa amesema kuwa jukumu kubwa la Taasisi hiyo ni kuhakiki vipimo na kuhakikisha vinatumika kwa usahihi na pia kuangalia ni kwa namna gani bidhaa mbalimbali zinafungashwa ili mtumiaji wa mwisho apate kilicho sahihi.
Aidha amesema kuwa watahakikisha wanafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na kamati hiyo ili kuhakikisha watanzania wote wanapata haki zao kupitia Taasisi hiyo kutokana na majukumu waliyopewa.