TAMISEMI BINGWA WA MCHEZO WA DARTS - SHIMIWI

Na. Asila Twaha, Iringa

Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeibuka bingwa  wa mchezo wa vishale (Darts) katika mashindano ya 37 ya shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yaliyohitimishwa Oktoba 14, 2023 Mkoani Iringa.

TAMISEMI Sports Club imepata ubingwa huo kupitia mchezaji wake Adelina Nyoni aliyeibuka kidedea katika mchezo huo na kuifanya timu hiyo kutembea kifua mbele katika mchezo wa dart huku ikishika nafasi ya pili kwa upande wanawake kupitia mchezo wa drafti.

Akihairisha michezo hiyo Katibu Tawala Mkoa wa Iringa Mhandisi Leonald Masanja alisema licha ya mashindano hayo kujenga afya kwa watumishi na kukuza ushirikiano miongoni mwa washiriki pia ilikuwa ni fursa nzuri kwa wakazi wa Iringa kufanya biashara kwa wingi kupitia uwepo wa ugeni wa washiriki wa mashindano hayo.

Sanjari na hilo, amewashukuru watumishi hao kwa ushiriki wao katika masuala ya kijamii katika kipindi chote walichokuwa mkoani hapo ambapo walitembelea vituo vya watoto wenye uhitaji maalum vya Tosamaganga, Faraja, Amani na kituo cha Huruma pamoja na kutembelea hifadhi ya Taifa ya RUAHA.

Akizungumza na washiriki wa mashindano hayo Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Rais - TAMISEMI Bw. Stanley Ngozi amewataka watumishi hao kuendelea kufanya mazoezi na kuhamasisha   watumishi wengine kufanya mazoezi  ili kujenga afya ya akili na mwili itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mashindano hayo ya 37 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali yaliyohitimishwa Oktoba 14, 2023 yalizinduliwa Septemba 4, 2023 yakiwashirikisha zaidi ya watumishi 2800.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post