KILELE CHA MAHAFALI YA 57 SHULE YA SEKONDARI KIBAHA

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Bw. Anathe Nnko akisisitiza jambo kwa wanafunzi wa kidato cha nne ambao wanatarajia kuanza mitihani ya Taifa ya kidato cha nne tarehe 13/11/2023 hadi 30/11/2023. Wengine ni viongozi wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Bodi ya Michezo ya Kubahatisha na wageni mbalimbali.

***********************

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Bw. Anathe Nnko leo tarehe amewataka wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Taifa ya kumaliza kidato cha nne ambayo itaanza tarehe 13/11/2023 hadi 30/11/2023 kuendelea kujiandaa ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao.

“Nawatakia mitihani mema, mkijiamini mtafanya vizuri, endeleeni kujiandaa vizuri,” amesema Bw. Nnko.

Katika hatua nyingine, Bw. Nnko amewashukuru Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) kwa kutoa msaada wa kisima cha kuhifadhia maji lita laki moja na matenki matano ya maji yenye uwezo wa kuhifadhi lita elfu kumi kila moja, kwa ajili ya huduma ya maji kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibaha.

Katika mahafali hayo, pia, Bw. Nnko amewashukuru walimu wa Shule ya Sekondari Kibaha kwa kuwa na malengo makubwa ya kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri katika mitihani mbalimbali.

Mgeni rasmi katika mahafali ya 57 ya kidato cha nne yaliyofanyika katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Bw. James Mbalwe amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidi ili waweze kufikia malengo yao.

Pia, Bw. Mbalwe amewataka wanafunzi hao waendelee kuwa na nidhamu kwakuwa nidhamu ni msingi wa mafanikio.

Naye, Mwenyekiti wa Wazazi Shule ya Sekondari Kibaha, Prof. Anthony Sangeda pamoja na kuwashukuru walimu, wazazi na wanafunzi wa shule hiyo, amewaomba wazazi waendelee kuwaombea wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne ili waweze kutimiza malengo yao.

“Wanangu moto ni single digit (daraja la kwanza lenye tarakimu moja) Mungu awasaidie kama moto wetu unavyosema. Wazazi muendelee kuwaombea watoto wetu ili watimize malengo yao. Kwa vijana wa kidato cha nne tunawaombea, tunaomba muendelee kupambana kama ambavyo mmeahidi, tunawatakia heri watoto, muendelee kushikamana, muwe kitu kimoja na tupo pamoja nanyi,” amesema Prof. Sangeda.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Elimu, Shirika la Elimu Kibaha, Bw. Fidelis Haule amewashukuru walimu wa Shule ya Sekondari Kibaha kwa kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri katika masomo pamoja na wazazi kwa kuweza kujitolea kwa hali na mali ili kuwezesha mafanikio shuleni.

Bw. Haule amemshukuru mgeni rasmi, Bw. James B. Mbalwe kwa kutoa msaada wa upatikanaji maji ya kutosha katika shule hiyo kwani mkono utoao ndio mkono upokeao.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwanalugali, Bw. Shomari Mguta amewashukuru walimu kwa malezi bora kwa wanafunzi wa Shule hiyo, lakini pia amefurahishwa na wanafunzi kuwa na nidhamu nzuri kwa jamii inayoizunguka Shirika la Elimu Kibaha.

Makamu Kaka Mkuu Mstaafu, Gration Sangeda akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wenzake, amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) kwa kutoa msaada wa kisima na matenki ya maji wenye jumla ya Shilingi 64,656,520. Pia wamewashukuru walimu na wafanyakazi wote wa Shule ya Sekondari Kibaha kwa kuwawezesha kufika hapo walipo
Mgeni rasmi katika mahafali ya 57 ya kidato cha nne, Shule ya Sekondari Kibaha, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Bw. James Mbalwe akizungumza katika kilele cha mahafali ya wanafunzi wa kidato cha nne ambao wanatarajia kuanza mitihani ya Taifa tarehe 13/11/2023 hadi 30/11/2023. Wengine ni viongozi wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Bodi ya Michezo ya Kubahatisha na wageni mbalimbali.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibaha inayomilikiwa na Shirika la Elimu Kibaha wakiwa kwenye kilele cha mahafali ya 57 ya shule hiyo ambayo yanafanyika katika viwanja vya Shirika.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Elimu, Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Bw. Fidelis Haule akitoa maelezo kwa mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, Bw, James Mbalwe pamoja na wageni wengine waalikwa katika kilele cha Mahafali ya 57 ya kidato cha nne yaliofanyika katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibaha inayomilikiwa na Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Bw. Geoarge Kazi akitoa taarifa ya shule hiyo kwa mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kuhabatisha Tanzania, Bw. James Mbalwe pamoja na wageni mbalimbali. Wengine ni viongozi wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Bodi ya Michezo ya Kubahatisha na wageni mbalimbali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post