VITI MAALUM VIFUTWE - MTANDAO WA WANAWAKE, KATIBA NA UONGOZI

 

Na Deogratius Temba

Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uongozi na Uchaguzi, ambao wamekuwa wakidai na kushawishi mabadiliko ya kisera, kisheria na kimuundo ili kutoa nafasi sawa kwa wanawake kushiriki kwenye nafasi za uongozi katika nyanja mbalimbali wametoa msimamo wao juu ya uwepo wa Viti Maalum katika nafasi za uongozi wa kisiasa. 


Mara baada ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kuteua Kikosi Kazi cha kukusanya maoni na kuyachakata juu ya namna ya kukuza Demokrasia nchini, Kikosi kazi ilichofanya kazi chini ya Uenyekiti wa Prof. Rwekaza Mkandala,  pamoja na kwamba Mtandao waliwasilisha maoni yao kwa kikosi kazi, moja ya pendekezo lao kama msimamo ni kuhusu muundo wa Viti maalum vya Ubunge, udiwani na Halmashauri za Vijiji na Kamati za Mitaa unaotumika hivi sasa. 

Wanamtandao wa Wanawake, Katiba, Uongozi na Uchaguzi ni muunganiko wa asasi za kiraia zaidi ya 200 ulioanzishwa mwaka 2011, ulishauri kwamba mfumo wa Viti Maalum uliopo sasa ufutwe katika ngazi zote za uongozi.  Kwa mantiki hiyo, kusiwepo na Viti Maalum vya wanawake.

Katika Mapendekezo ya Mtandao, wanasema kwamba: “ Licha ya kwamba, wadau walishauri kuondolewa kwa mfumo wa Viti Maalum, Kikosi Kazi kiliamua Mfumo wa Viti Maalum uendelee bila kutoa sababu za msingi za kuendeleza huu mfumo” inaeleza sehemu ya Taarifa ya Mapendekezo ya Mtandao wa wanawake na Katiba na kuongeza kuwa:

“Kikosi Kazi kilipendekeza kwamba, Wabunge wa Viti Maalum waitwe Wabunge wa Taifa na Madiwani waitwe Madiwani wa Wilaya. Vile vile Kikosi Kazi kilipendekeza Sheria ya Mfuko wa Uchaguzi ibadilishwe ili Wabunge wa Viti Maalum wafaidike nao kama Wabunge walioteuliwa kwa kupitia majimbo ya Uchaguzi. Na kwamba kuweko kwa mwongozo wa kisheria wa uteuzi wa wagombea na uchaguzi wa viongozi ndani ya Vyama vya Siasa ikiwemo wabunge wa Viti Maalum ili kusaidai uteuzi na uchaguzi wa haki na huru” pendekezo hili la Kikosi kazi, Mtandao unalikataa.

Mtandao wa wanawake na Katiba hawakubaliani pia  na maoni ya Kikosi kazi kwamba;  mfumo wa viti maalum uliopo sasa uendelee kutumika kama njia ya kupata uzoefu na kisha kupisha wanawake wengine wenye nia ya kuongeza uzoefu na ujuzi wa masuala ya siasa,

“Kwetu sisi Wanamtandao wa Wanawake, Katiba, Uongozi na Uchaguzi, tunaona pendekezo la kuendeleza Viti Maalum ambavyo sisi kama wadau tunaoathirika na mfumo huu uliopo ambao tunaona umejaa ubaguzi na udhalilishaji wa Kijinsia, tunashauri ubadilishwe au kuondolewa kabisa” inasema sehemu ya Mapandekezo ya Mtandao. 


Lakini pia, wanamtandao wa wanawake Katiba, Uongozi na Uchaguzi, wanasema kwamba,  kuendeleza mfumo wa Viti Maalum wa sasa ni kuijengea jamii imani kwamba, wanawake bado hawana uwezo, uzoefu, wala ujuzi wa masuala ya siasa, na kwamba  wengi ikiwa ni pamoja na hao walioko kwenye uwanda wa siasa tayari, kwamba wanahitaji takriban miaka kumi ya kujenga uwezo huo ili kuwapisha wengine wanaowania kuingia kwenye uwanda wa siasa. 


Ni muhimu kujenga fikra chanya kuhusu uwezo wa wanawake, na pia kutokuwaunganisha kwenye kapu moja na Makundi Maalum. Wanawake sio wote ni makundi maalum kwa sababu hata wanaume baadhi yao wapo kwenye kundi maalum. 


Tafsiri ya Mtandao wa wanawake, Katiba Uongozi na Uchaguzi juu ya kuendeleza mfumo wa Viti Maalum, ni la kuturudisha nyuma, na kupuuza hazina ya ujuzi, uwezo  ulioko miongoni wa wanawake wengi kwenye masuala ya siasa na uongozi. 


Nchi yetu inatakiwa kuweka mazingira salama, wezeshi na kuondoa vikwazo kwenye michakato ya uchaguzi ili kuwapa nafasi wanawake washindane na wanaume. Tunapoelekea kwenye chaguzi za serikali za Mitaa mwaka 2024, ni muhimu kuanza kujiandaa kuweka mifumo rafiki ya uchaguzi kwa wanawake ili wagombee na wanaume, na wapigiwe kura ambazo sio za huruma au za kupewa kwa sababu wao ni wanawake.


Ili kushughulikia usawa wa kijinsia katika uongozi, serikali ilifanya marekebisho ya Sheria ya Mamlaka za Serikali za Wilaya (1982) na marekebisho Na.4 ya mwaka 2000 katika kifungu cha 35 ili kuanzisha jitihada za makusudi za kuongeza uwakilishi wa wanawake katika serikali za mitaa ambapo wanawake wanapaswa kufikia theluthi moja ya wajumbe wa mabaraza.


Katika ngazi ya kijiji, wanawake wanapaswa kuwa asilimia 25 ya wajumbe wa Halmashauri ya kijiji ambayo kwa kawaida ina wajumbe 15 hadi 25. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa asilimia 30 ya viti maalum kwa wanawake Bungeni na asilimia 33.3 ya viti maalum katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Ingawa mafanikio makubwa yamepatikana, Serikali bado haijafikia lengo la Umoja wa Afrika la usawa wa kijinsia wa 50/50.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post