MAKADA WA CCM WAKUNWA UTEUZI WA MAKONDA... MGEJA AGUSWA SIASA ZA KIZAZI CHA 'DOT COM'


Paul Makonda

Na Suleiman Abeid, Shinyanga.

HALMASHAURI Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa imepongezwa kwa uamuzi wake wa kumteua Paul Makonda kuwa Katibu wa Itikadi na uenezi wa Taifa na kwamba uteuzi huo ni chaguo sahihi linaloendana na wakati uliopo hivi sasa.

Pongezi hizo zimetolewa leo mjini Shinyanga na makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo wamesema uteuzi huo unastahili kuungwa mkono na kila mwanachama wa CCM mwenye nia njema na chama chake.

Mbali ya pongezi hizo makada hao wamesema Makonda ni mmoja wa vijana hapa nchini ambao wamelelewa ndani ya Chama cha Mapinduzi tangu akiwa upande wa Jumuiya ya vijana wa CCM na kwamba wana CCM wana kila sababu za kuunga mkono uteuzi huo na kumpa ushirikiano wa kutosha.

Wamesema hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi kwa kuangalia matukio yake yaliyopita na kwamba hakuna binadamu ye yote aliyekamilika hivyo wana CCM wanapaswa kushimakamana kwa pamoja katika kukijenga chama chao kwa nguvu zote ili kiendelee kukubalika na watanzania wakati wote.

Khamis Mgeja aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga na Bernard Itendele mkuu wa wilaya na katibu wa CCM mstaafu mbali ya kupongeza uteuzi huo wametoa wito kwa wana CCM kumpa ushirikiano wa kutosha ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake katika nafasi aliyoteuliwa.

“Binafsi nichukue nafasi hii kuipongeza Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa uteuzi ilioufanya kwa ndugu yetu Makonda, kwa kweli naamini ni chaguo sahihi la CCM na limekuja kwa wakati muafaka, na hatokuwa mgeni sana kwenye nafasi hii maana anakijua vizuri Chama na hata Serikali,”

“Niwaombe wale wenye mashaka naye waondoe shaka kabisa, kikubwa niwashauri wana CCM wasahau yote yaliyopita na tugange yajayo, wakumbuke hakuna binadamu aliyekamilika, hivyo uteuzi huu umekuja wakati muafaka maana Makonda atakwenda na wakati tulionao hivi sasa,” amesema Mgeja.

Mgeja amesema ili Makonda aweze kuwa na mafanikio makubwa ni lazima apate ushirikiano katika kukijenga Chama na tumuunge mkono na kwamba peke yake hawezi kufanya jambo lolote na kwamba asihukumiwe kwa mambo yaliyopita.

“Lakini pia niwapongeze viongozi wengine waliopita kwenye nafasi hiyo, waelewe tu uongozi katika nchi yetu ni wa kuwapokezana kijiti, dada yetu Sophia Mjema amefanya kazi kwa kiwango chake na sasa anaenda kumsaidia Rais Samia, hivyo na yeye tumtakie kila la kheri,” ameeleza Mgeja.

Hata hivyo Mgeja amewataka wana siasa wote nchini hivi sasa kuzisoma alama za nyakati na kwamba sasa hivi asilimia 85 ya wananchi ni kizazi kipya hivyo uelewa wao umekuwa ni mkubwa na hivyo siasa za leo siyo zile za jana, tuna kizazi cha “Dot Com” hivyo lazima waongozwe kulingana na upepo unavyokwenda.

Kwa upande wake Bernard Itendele amesema uteuzi wa Makonda utakiwezesha chama kwenda na wakati hasa ikizingatiwa kuwa yeye ni miongoni mwa vijana hapa nchini wenye uwezo mzuri wa kiuongozi na wachapakazi.

“Hatuna sababu ya kuhofia uteuzi wa Makonda, huyu ni kijana amekulia ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) lakini pia amepata fursa ya kuwa kiongozi ndani ya Serikali yetu hivyo anao uwezo mkubwa wa kufanya vizuri katika nafasi aliyoteuliwa hivi sasa,” ameeleza Itendele.

Joseph Maganga mkazi wa Ibinzamata Manispaa ya Shinyanga amesema Makonda ni moja ya vijana wenye uwezo mkubwa wa kuchapa kazi na kwamba wana CCM wategemee matokeo mazuri kwenye utendaji kazi wake na wamuunge mkono badala ya kumkwamisha.

Zipora Pangani ambaye pia ni mmoja wa wakuu wa wilaya wastaafu hapa nchini amesema Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inastahili pongezi kwa kumteua Makonda katika nafasi ya uenezi ndani ya Chama Cha Mapinduzi.

“Makonda ni shupavu, maana kila eneo alilopewa kufanya kazi alifanya vizuri, ni mtu mwenye kujituma, mwenye kusimamia jambo analoliamua hana tabia ya kurudi nyuma kwenye jambo aliloamua na anajua kukipigania chama,”

“Na hata alipokuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam alionesha uwezo wake wa kiuongozi, maana hata kwenye kusaidia, alisaidia makundi mengi ikiwemo ya wale wasiojiweza, akinamama wajane na hata vijana wenzake, ni mtu msikivu na mkimya na anapokuwa na malengo anakuwa makini sana,” ameeleza Pangani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments