WAZIRI BASHUNGWA: BARABARA APP SULUHU LA MIUNDOMBINU YA BARABARA
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akizunguma na menejimenti ya Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo iliyo chini ya Wizara ya Ujenzi, jijini Dodoma


Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Eng. Aisha Amour, akizungumza mbele ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), jijini Dodoma.


Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara, Eng. Rashid Kalimbaga, akiwasilisha taarifa ya Majukumu ya Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), kwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (hayupo pichani), katika kikao kazi na Bodi hiyo iliyo chini ya Wizara ya Ujenzi, jijini Dodoma


Sehemu ya menejimenti ya Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), wakisikiliza maelezo kutoka kwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (hayupo pichani), katika kikao kazi kilichowakutanisha katika ofisi za Bodi hiyo jijini Dodoma Septemba 27, 2023. Wa kwanza Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Ludovick Nduhiye.

...........

Na.Mwandishi Wetu-DODOMA

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amewataka wananchi kutoa taarifa za hali ya barabara nchini kupitia mfumo wa kieletroniki wa ‘Barabara App’ ili hatua za haraka kwa barabara zinazohitaji matengenezo ziweze kuchukuliwa.

Amesema kupitia mfumo huo, watumiaji wa barabara wanaweza kushiriki katika kusimamia miundombinu ya barabara katika maeneo wanayoishi au kupita kwa kutuma taarifa muhimu za hali ya barabara katika Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), ambapo Bodi hiyo itawasilisha mahala husika katika Taasisi ya Wakala ya Barabara Nchini (TANROADS) na Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

Ametaja miongoni mwa taarifa hizo ikiwemo barabara kujifunga, daraja au kalvati kubomoka/ kuzolewa na mafuriko, mashimo hatarishi barabarani, kazi kufanyika chini ya kiwango, mitaro kuziba na hujuma zozote zinazofanyika katika miundombinu ya barabara.

Waziri Bashungwa ameyasema hayo Septemba 27, 2023 jijini Dodoma wakati akihitimisha ziara yake katika Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) ambapo Waziri huyo alipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo.

“Niwaombe watanzania kutumia mfumo huu unaomwezesha mwananchi kutoa taarifa ya hali ya miundombinu ya barabara yenye changamoto, au hujuma yoyote maeneo anayoishi”, amefafanua Bashungwa.

Bashungwa ameongeza kuwa lengo la kuwa na mfumo huo ni kuipunguzia Serikali gharama kubwa za matengenezo ambayo ingeia kutokana na uchelewaji wa matengenezo hayo.

Aidha, Bashungwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga vyema kuhakikisha Taasisi ya Wakala ya Barabara Nchini (TANROADS) inayosimamia barabara kuu na za mikoa na ile ya Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), inayosimamia barabara za Halmashauri/ Wilaya wanajipambanua zaidi katika kuhudumia barabara zote nchini.

Amewataka watanzania kuwa na imani na taasisi hizo katika kuhudumia na kusimamia mtandao a barabara nchini kwa mujibu wa mgawanyo wa majukumu yao.

“Ningependa kuwajulisha watanzania kuwa huko nyuma kulikuwa na maombi makubwa ya barabara ambazo zipo kwenye wilaya zetu ili zipandishwe hadhi kuja TANROADS, lakini hivi sasa hilo hitaji ni kama limeisha kwasababu TARURA imekwisha jengewa uwezo na kuimarishwa mfuko wake”, amefafanua Bashungwa.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo, Kaimu Mtendaji wa RFB Eng. Rashid Kalimbaga, ameeleza kuwa mbali na mfumo wa kieletroniki wa kufuatilia barabara Bodi imeimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuzuia matumizi mabaya ya fedha.

Ameongeza kuwa kuimarika kwa mifumo hiyo kutaziba mianya ya uvujaji wa mapato pamoja na uchakachuaji katika ujenzi na matengenezo ya barabara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post