MANISPAA YA SHINYANGA YAADHIMISHA WIKI YA ELIMU YA WATU WAZIMA, MKURUGENZI WA BSL ASISITIZA WAZAZI KUWAENDELEZA WANAFUNZI WALIOKATISHA MASOMO

Kuelekea kilele cha maadhimisho ya wiki ya Elimu ya watu wazima nchini kesho Septemba 28, 2023 Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga jana imeadhimisha wiki hiyo kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa Elimu.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Mgeni Rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa BSL Investimenti Company Limited Peter Frank (Mr. Black) amewasihi wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata elimu kwa manufaa yao ya baadae.

Amesema licha ya changamoto zinazojitokeza ikiwemo watoto wa kike kukatishwa masomo kwa sababu ya ujauzito siyo chanzo cha wao kufikia mwisho wa kutimiza malengo yao hivyo ni vyema kupatiwa fursa hiyo kupitia taasisi mbalimbali za elimu ya watu wazima.

“Tunashiriki maadhimisho haya kwasababu tunahitaji kuona elimu inafika sehemu husika, kushindwa kwa watoto wetu kuendelea na masomo ama kwa sababu ya umbali, ujauzito au sababu yeyote si mwisho wa wao kufikia malengo yao katika elimu”, amesema Frank

Awali, akisoma risala mbele ya Mgeni Rasmi Afisa Elimu ya watu wazima Divisheni ya elimu Msingi na Sekondari katika Manispaa ya Shinyanga Mwalimu Judith Kagembe amebainisha mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa katika taasisi hiyo ikiwemo watu wazima wasiojuwa kusoma, kuhesabu na kuandika kuwa na hamasa ya kujifunza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya afya, elimu na uchumi katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Lubaga Mheshimiwa Ruben Dotto amesema Baraza la Madiwani litaendelea kuishauri serikali kuendelea kuwekeza katika elimu ya watu wazima ili kuleta msukumo zaidi.

Maadhimisho hayo ngazi ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga yamefanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo katika shule ya Msingi Buhangija, yakiongozwa na kauli mbiu inayosema kukuza uwezo wa kusoma na kuandika kwa ulimwengu unaobadilika ili kujenga misingi ya jamii endelevu na yenye amani.

Washiriki waliohudhuria maadhimisho hayo ni wadau mbalimbali wa elimu ya watu wazima wakiwemo wajasiriamali, vyuo vya ufundi stadi, wanafunzi wa BSL Nhelegani, wanafunzi wa MEMKWA na wanafunzi wenye mahitaji maalumu wa Shule ya Msingi Buhangija.
Mgeni rasmi Mkurugenzi wa BSL INVESTMENT COMPANY LIMITED Peter Frank Mr. Black akizungumza wakati wa maadhimisho hayo
Mgeni rasmi Mkurugenzi wa BSL INVESTMENT COMPANY LIMITED Peter Frank Mr. Black akizungumza wakati wa maadhimisho hayo
Afisa Elimu ya Watu wazima Divisheni ya Elimu msingi na Sekondari katika manispaa ya Shinyanga Mwalimu Judith Kagembe akizungumza wakati wa maadhimisho hayo


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post