WATOTO WAWILI WA FAMILIA MOJA WAFARIKI KWENYE BWAWA KISHAPU


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Watoto wawili Meckline Dioniz (6) na Mbalu Dioniz (3) wa familia moja wakazi wa kitongoji cha Nkongolo Kijiji cha Kabila kata ya Mondo wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga wamefariki dunia baada ya kuzama katika bwawa la maji.


Inaelezwa kuwa tukio hilo limetokea jana Jumatano Septemba 13,2023 majira ya saa nne usiku.

Akizungumza na Malunde 1 blog, Diwani wa kata ya Mondo ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, William Jijimya amesema tukio hilo la kusikitisha limetokea wakati wazazi wa watoto hao wakiwa msibani.


“Kulikuwa na msiba hapa Kijiji cha Kabila, wazazi walienda msibani, walivyorudi nyumbani usiku hawakuwaona watoto, juhudi za kuwatafuta zikaanza kufanyika, wanakijiji wakakusanyika na kuanza kutafuta watoto, wakaona mtoto mmoja anaelea juu ya maji na baadae wakaopoa mwili wa mtoto mwingine kwenye bwawa hilo. Watoto hao inaonekana walienda kucheza/kuogelea katika bwawa baada ya wazazi wao kuondoka”,ameeleza Jijimya.

“Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola vimefika hapa,miili ya watoto imefanyiwa uchunguzi kwa ajili ya taratibu zingine”,amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

“Watoto hao waliachwa nyumbani na wazazi wao, waliporudi wakawakosa hao watoto na baadae wakabaini mtoto aitwaye Mbalu Dioniz amefariki kwenye dimbi la maji huku mtoto mwingine akiwa hajulikani alipo…Jitihada za wananchi kwa kushirikiana na Jeshi la polisi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji zikaendelea kumtafuta mtoto mwingine”,ameeleza Kamanda Magomi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post