TBS YATOA ELIMU KWA WANANCHI KWENYE MAONESHO YA NANENANE MWANZA

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Ziwa limeshiriki maonesho ya wakulima Nanenane 2023 katika uwanja wa Nyamhongolo jijini Mwanza, kwa lengo la kutoa elimu kwa wadau na wananchi kuhusu udhibiti na ubora wa bidhaa mbalimbali.

Meneja TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka amesema shirika hilo limetumia fursa ya maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali wakiwemo wazalishaji wa mazao ya chakula yatokanayo na kilimo, ufugaji pamoja na uvuvi ili kuhakikisha wanazalisha bidhaa zinazokidhi viwango.

“Kaulimbiu mwaka huu inasema ‘vijana na wanawake ni msingi imara wa uendelevu katika uzalishaji wa mifumo ya chakula’, hivyo TBS tuna jukumu la kuhakikisha chakula kinachozalishwa kinakidhi matakwa ya viwango na ni salama kwa matumizi ya bindamu” amesema Kanyeka.

Kanyeka ameongeza kuwa kupitia maonesho hayo, TBS pia inatoa elimu kwa wananchi ili kutambua bidhaa zenye ubora, zinazofaa kwa matumizi na zilizopigwa marufuku ikiwemo vipodozi ili kuepuka matumizi yake kwani zina madhara makubwa kiafya.

Naye Afisa Mkaguzi TBS Kanda ya Ziwa, Musa Mayala amesema pia wanatoa elimu kwa wazalishaji na wauzaji wa bidhaa za vipodozi na chakula ili kuhakikisha wanadhibiti ubora wa bidhaa zao na kuepuka kuuza bidhaa zilizopigwa marufuku, zilizoisha muda huku pia wakizingatia utunzaji bora wa bidhaa ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea kwa watumiaji/ walaji.

Mayala ameeleza kuwa pia TBS inawahamasisha wajasiriamali kusajili bidhaa zao na kupata nembo ya ubora huku akiwatoa hofu kwamba Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuwainua wajasiriamali wadogo kwa kuwapa fursa ya kupata nembo ya ubora bure kwa kipindi cha miaka mitatu.

“Tunalenga kuwainua wajasiriamali wadogo kutoka hali ya chini kwenda hali ya juu ambapo Serikali imetoa utaratibu wa kuwasaidia kufanya shughuli zao kwa miaka mitatabu bila kulipia gharama za nembo ya ubora. Pia tunatoa mafunzo ya aina mbalimbali kuhusu namna ya kuandaa bidhaa zenye ubora na kudhibiti madhara yanayoweza kuwapata watumiaji” amesema Mayala.

Mmoja wa wananchi waliotembelea banda la TBS kwenye maonesho ya Nanenane Nyamhongolo jijini Mwanza ni David Maduhu ambaye ameshauri shirika hilo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa bidhaa zinazozalishwa ama kuingizwa nchini ili kuhakikisha wazalishaji wanazingatia ubora uliokusudiwa.

“Nafurahi pia wamenipa vipeperushi vyenye orodha ya bidhaa ambazo hazipaswi kuwa sokoni. Nashauri waendelee kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa bidhaa zinazosajiliwa na kupewa nembo ya ubora ili kuhakikisha wazalishaji wanazingatia ubora ule ule uliokusudiwa” amesisitiza Mayala.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Meneja TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka akieleza kuhusu ushiriki wa shirika hilo kwenye Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kanda ya Ziwa Magharibi kwenye uwanja wa Nyamhongolo jijini Mwanza yakishirikisha mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera.
Meneja TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka akizungumza kwenye Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Nyamhongolo jijini Mwanza.
Afisa Mkaguzi TBS Kanda ya Ziwa, Musa Mayala akieleza namna shirika hilo linavyowasaidia wajasiriamali kuboresha bidhaa zao ili kukidhi viwango na kupata nembo ya ubora.
David Maduhu ambaye no mmoja wa wananchi waliotembelea banda la TBS kwenye Maonesho ya Nanenane yanayofanyika uwanja wa Nyamhongolo jijini Mwanza akiwa na vipeperushi mbalimbali vyevye elimu kuhusu bidhaa zenye ubora na zilizopigwa marufuku sokoni.
Wananchi wakipata elimu kwenye banda la TBS kwenye Maonesho ya Nanenane 2023 Nyamhongolo jijini Mwanza.
Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka (katikati) na Afisa Afisa Mkaguzi TBS Kanda ya Ziwa, Musa Mayala (kushoto) wakitoa elimu kwa mmoja wa wananchi waliotembelea banda la shirika hilo kwenye maonesho ya Nanenane Nyamhongolo jijini Mwanza.
Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka (kushoto) akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyamuge waliotembelea banda la shirika hilo.
Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown Kanyeka (wa pili kushoto waliokaa) na Afisa Afisa Mkaguzi TBS Kanda ya Ziwa, Musa Mayala (wa kwanza kushoto waliokaa) wakitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyamuge.
Wanafunzi wakipata elimu kwenye banda la TBS kwenye Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Ziwa Magharibi yanayofanyika uwanja wa Nyamhongolo jijini Mwanza yakishirikisha mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera kuanzia Agosti Mosi hadi Agosti 08, 2023.
PIA SOMA>>> HABARI ZAIDI HAPA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post