BIBI WA MIAKA 92 AUAWA KISHA KUNYOFOLEWA MACHO


Nyumba aliyokuwa kikongwe huyo

Kikongwe Minza Maduhu mwenye umri wa miaka 92 mkazi wa mtaa wa Mwakiboro, Kata ya Bunamhala wilaya Bariadi mkoani Simiyu ameuawa na kisha kunyofolewa macho yote mawili.

Tukio hilo limetolewa usiku wa kuamkia  Agosti 1 na bibi huyo alikuwa akiishi peke yake ambapo mmoja wa wajukuu ambaye ndiye aliyekuwa akimpikia amesema alipomaliza kupika chakula cha jioni alimuaga bibi yake na asubuhi alipoenda alikutana tu mwili uliotapakaa damu kitandani.

"Akaniambia haya mjukuu wangu nenda ila kesho uwahi kuja asubuhi unga umeisha ndani ukasage, mida ya saa moja nikawa nimefika hapa nikaanza kubisha hodi bibi haitiki mara nikaangalia pale mlangoni pamefungwa kwa nje nikafungua nikapita mle ndani nikaona tu mguu wa bibi umening'inia kitandani, ikabidi niwashe tochi nimlike nijue nini kinaendelea kumlika kitandani nikakutana na damu mwili ukaishiwa nguvu nikaanza kutetemeka," amesema Anna Maduhu,Mjukuu wa marehemu .

Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Kata ya Bunamhala amesema tangu Januari 2023 mpaka Augosti 1, 2023 ndilo tukio la kwanza kwenye Kata huku akilaani tukio hilo na kuiomba jamii kuwa karibu na wazazi wao huku mwenyekiti wa mtaa wa Mwakiboro akisema tayari wameanza kupiga kura za maoni kubaini wahusika wa tukio hilo

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Bunamhala amesema mwili wa bibi huyo ulikuwa na majeraha na macho yakiwa yametobolewa huku akiongeza kuwa majeraha yamesababishwa na kitu chenye ncha kali na sababu za kifo zikitajwa kuwa ni kuvuja kwa damu nyingi.

CHANZO - EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments