WANANCHI WA KIJIJI CHA KILOLELI - KISHAPU WAHAMASIKA UJENZI WA MATUNDU YA VYOO

Na Mwandishi wetu _ Malunde 1 blog

WANANCHI wa kijiji cha Kiloleli halmashauri ya Kishapu mkoani Shinyanga wamefanikiwa kuanzisha ujenzi wa matundu 24 ya vyoo na chumba kimoja cha kujistiri wanafunzi wa kike wakati wa hedhi na kuondoa changamoto iliyokuwa ikiwakabili shuleni hapo.

Ujenzi huo umetokana na wanakituo cha taarifa na maarifa waliojengewa uwezo na Mtandano wa Jinsia Tanzania (TGNP) kuibua changamoto zinazowakabili katika sekta mbalimbali ikiwemo Elimu,Afya na Maji.

Wakiongea na waandishi wa habari waliofika katika kijiji hicho jana tarehe 12/08/2023 kuona mafanikio ya wananchi ambayo yaliibuliwa na wanakituo cha taarifa na Maarifa kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto shuleni.

Mwanakituo cha taarifa kijiji cha Kiloleli Helena Makele amesema wanafunzi wamekuwa wakijisaidia vichakani baada ya matundu ya vyoo manane kujaa na hayatoshelezi kwa wanafunzi waliopo hivyo wakahamasishana wao na baadaye kulipeleka kwenye mkutano wa hadhara wananchi wakakubali kuchangia fedha.

Mwanakituo cha taarifa na Maarifa kutoka Kiloleli Joseph Solea amesema waliona changamoto kubwa ni kukosa matundu ya vyoo maana yaliyopo yalikuwa yamejaa wakajadiliana , wakahamasisha  jamii ikakubali kuanza kutoa sh 1000 na kuchimba shimo kwa kujitolea na wakaona haitoshi wakarudi tena kuchangia sh 2000 wanafunzi wakihitaji huduma wanajitafutia mahali popote.

Mkazi wa kijiji cha Kiloleli Martha Ngwelu amesema waliibua ujenzi wa vyoo kutokana na vyoo vyenye matundu manane kujaa na havikutosheleza kutokana na idadi ya wanafunzi hivyo waliitishwa mkutano wa hadhara na kukubaliana kuanzisha ujenzi huo.

“Hamasa ilitoka kwa wanakituo cha taarifa na maarifa baada ya wao kuanzisha harambee ya mchango na kutoa sh 50,000 na mifuko ya Saruji mitano lakini sisi mara nyingi tulikuwa tukiliongelea kwenye mikutano ya hadhara bila mafanikio wao wametuhamasisha vyoo vimeanza kujengwa”amesema Ngwelu..

Mwalimu mkuu msaidizi wa shule ya Msingi Kiloleli Juliana Petro amesema shule hiyo ina wanafunzi 997 changamoto iliyopo ni ukosefu wa matundu ya vyoo na wanafunzi wanapitwa na masomo kwa kushelewa chooni sababu ya matundu yaliyokuwepo yamejaa na machache na sasa wanajisaidia vichakani.

“Matundu 24 ya vyoo yaliyojengwa yatasaidia kuondoa changamoto iliyokuwepo awali kulikuwa hakuna chumba cha kujistiri wanafunzi wa kike sasa kimewekwa jamii imeanza kupata uelewa kwani uwiano unaotakiwa wanafunzi 25 tundu moja kwa wakiume na wa kike wanafunzi 20 tundu moja”amesema Juliana Petro.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kiloleli Kuhwema Mshala amesema changamoto zilizokuwepo shuleni matundu ya vyoo yalikuwa hayatoshi na yamejaa wakaamua kuwaita vituo vya taarifa na maarifa na wananchi wakazungumza kwenye mkutano wa hadhara na kukubaliana kituo cha taarifa na maarifa kutoa sh 50,000 na mifuko ya Saruji mitano.

“Wananchi walikubaliana kuchangia sh 2000 tukanunua nondo na Saruji na kujenga bamba na wananchi wakachimba tena karo na kuleta mchanga nguvu kazi na kikao cha Maendeleo ya kata (WDC) walitoa mifuko 30 ya Saruji na matofali yakavyatuliwa kwaajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo”

Mashara amesema serikali ya kijiji ilitoa sh 600,000 na Sungusungu walitoa sh 500,000 na ujenzi ukaanza na wanaiomba serikali waongeze fedha waweze kupaua lakini wakiona wanachelewa watajitahidi wakamilishe wenyewe.

Mtendaji wa kijiji Nicholaus Mzirai amesema halmashauri ya kijiji hicho wamepata sh Millioni 1.3 zitokanazo na ushuru wa zao la pamba na wamefanya matumizi ya sh 500,000 kwaajili ya uendelezaji wa ujenzi wa matundu ya vyoo na michango ya wananchi ilipatikana sh 700,000.
Choo cha zamani shule ya msingi Kiloleli.

Matundu ya vyoo cha zamani shule ya msingi Kiloleli.Mkazi wa kijiji cha Kiloleli Martha Ngwelu Akizungumza na waandishi wa habari.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kiloleli Kuhwema Mshala Akizungumza.

Mwalimu Mkuu Msaidizi Shule ya Msingi Kiloleli Juliana Petro akizungumza.

Vyoo vipya  vyinavyojengwa shule ya msingi Kiloleli.


Vyoo vipya  vyinavyojengwa shule ya msingi Kiloleli.

Mtendaji wa kijiji Nicholaus Mzirai akizungumza na waandishi wa habari.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post