LEMBELI AWANYOSHEA KIDOLE VIONGOZI WA CCM KAHAMA KUMTUHUMU KUHUJUMU MBIO ZA MWENGE


Na Mwandishi wetu - Kahama
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kahama 2005-2015 James Lembeli amewashutumu viongozi wa CCM wilaya ya Kahama kumtuhumu kufanya njama za kuhujumu sherehe za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika kijijini kwake Mseki kata ya Bulungwa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga Julai 31, 2023 tuhuma ambazo amesema ni uzushi na uongo usio kifani.


Akizungumza leo kijijini kwake baada ya kurejea toka Dar es Salaam alikoenda kwa shughuli binafsi, Lembeli amesema shutuma hizo ambazo zilidai yeye kununua pombe zote za kijijini hapo kwa ajili ya kunywesha wananchi siku ya mkesha wa mwenge  wa uhuru kwa lengo la kuwazuia wasiende kwenye mkesha hivyo shughuli hiyo kushindwa kufanikisha malengo ni za uongo na ni uzushi usio na tija binafsi wala ya kisiasa.

"Michezo kama hiyo katika siasa za leo hailipi wala haimsaidii mhusika kujiimarisha kisiasa wala kijamii. Muhimu ni kijiamini na kufanya kazi uliyoomba ya kuwatumikia wananchi bila kujichanganya",amesema Lembeli.

Amesema yeye binafsi tangu jitihada zake za kugombea uenyekiti wa CCM mkoa zilipokwama, aliachana na harakati za kusaka uongozi ndani chama na kuelekeza nguvu zake katika masuala binafsi na amejikita zaidi kuwatumikia watanzania na walimwengu katika masuala ya uhifadhi na ulinzi wa mazingira ndani na nje ya Tanzania.


Amesema  kinachoendelea ni baadhi ya viongozi ndani ya CCM kumwogopa hivyo kila mara kumzushia mambo ya ajabu ajabu kwa lengo la kumchafua.

Lembeli amedai waliotoa pesa hiyo ni viongozi wenyewe wa CCM Wilaya ya Kahama na kuzituma kwa aliyekuwa diwani wa kata ya Bulungwa kwa jina Joseph Msaluta Msambusi ambaye akisaidiana na aliyekuwa katibu mwenezi wa kata hiyo Fredrick Maduka walisaidiana kununua hiyo pombe na kuratibu shughuli nzima ya unywaji wa pombe hiyo.


Amesema jambo hilo limemuhuzunisha kwa kuwa yeye binafsi anakubaliana na madhumuni ya kuwepo kwa mwenge wa uhuru na ameshiriki shughuli zote za mwenge wa uhuru tangu akiwa shule ya msingi hadi akiwa Mbunge.

Amewataka viongozi hao wasitumie madhaifu na mashindano yao ya kisiasa kumhusisha katika vitendo vya rushwa za kisiasa.


Lembeli amesema wakati tuhuma hizo zikitolewa yeye alikuwa Dar es Salaam kuhudhuria kikao cha Bodi ya Taasisi ya Jane Goodall Tanzania ambako yeye ni mwenyekiti.


Amemuomba Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita, kwa kutumia vyombo vyake vya  ulinzi na salama kuwahoji  Masaluta na Maduka na kwamba ni nani aliwapa pesa hizo na kwa madhumuni gani ili kumweka huru lakini pia wananchi ambao walisikitishwa na tuhuma hizo kwake (Lembeli).

Alipotafutwa na mwandishi wetu, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kahama, Thomas Muyonga ameeleza kushangazwa na madai hayo ya Lembeli akisema Mwenge wa Uhuru umeingia na kutoka salama wilayani Kahama na hakuna malalamiko yoyote.

"Hii ni habari mpya sijui chochote, shughuli za pale kwenye Mwenge zilienda vizuri hatuna malalamiko, Chama hakijapokea malalamiko kutoka kwa mtu yeyote, shughuli za Mwenge zilienda vizuri,Mwenge wa Uhuru  ulikuwa umejaa mwanzo mwisho Kahama na Bulungwa umetoka salama hatuna doa, wananchi wamefurahia mwenge wa uhuru, hizi habari mpya kwa kweli arudi kwa mtu aliyempa taarifa hizi. Mwenge wa Uhuru umeingia na kutoka salama kabisa wilayani Kahama",amesema Lembeli.

Hata hivyo akizungumza na Mwandishi wetu, Aliyekuwa diwani wa kata ya Bulungwa, Joseph Msaluta Msambusi amesema yeye ndiye alinunua pombe yenye thamani ya shilingi Laki tatu (300,000/= ) kwenye Mkesha wa Mwenge wa Uhuru kwa lengo la kukusanya wananchi kwenye mkesha huo ili waushangilie Mwenge wa Uhuru.

"Mimi Joseph Msaluta Msambusi nikiwa na Fredrick Maduka ndiyo nilinunua pombe kwa ajili ya kuwakutanisha wananchi ili Mwenge mkesha wa Mwenge uwe na watu wengi , watu wakeshe kwenye Mwenge wafurahie Mwenge , waushangilie Mwenge. Gharama ya pombe niliyonunua kwenye Mwenge ni shilingi 300,000/=",amesema Masaluta

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post