WAZIRI MKENDA AVITAKA VYUO VIKUU KUWAENDELEZA WANATAALUMA


Makamu Mkuu Chuo Kikuu Ardhi Prof. Evaristo Liwa akimuonyesha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda eneo litakalojengwa Kampasi ya Chuo Kikuu Ardhi wilayani Sengerema Mkoani Mwanza wakati wa ziara ya Waziri huyu.

Makamu Mkuu Chuo Kikuu Ardhi Prof. Evaristo Liwa akimuonyesha Mchoro Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (hayupo pichani) eneo litakalojengwa Kampasi ya Chuo Kikuu Ardhi wilayani Sengerema Mkoani Mwanza kitakavyokuwa chuo kitakapokamilika.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua eneo litakalojengwa Kampasi ya Chuo Kikuu Ardhi wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.


Makamu Mkuu Chuo Kikuu Ardhi Prof. Evaristo Liwa ,akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda kukagua eneo litakalojengwa Kampasi ya Chuo Kikuu Ardhi wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.

Na.Mwandishi Wetu-MWANZA

Wito umetolewa kwa vyuo vikuu nchini kuendeleza wanataaluma wake ili kuviwezesha kuwa na wahadhiri wa kutosha watakaokidhi mahitaji hasa wakati huu ambao zinakwenda kujengwa kampasi za vyuo vikuu katika mikoa mbalimbali.

Wito huo umetolewaJijini Mwanza na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda alipofanya ziara katika eneo litakalojengwa kampasi ya Chuo Kikuu Ardhi wilayani Sengerema ambapo amesema vyuo hivyo vinapaswa kuona umuhimu wa kuendeleza wanataaluma wake ili kuviwezesha kuwa nao wa kutosha na wenye wenye Umahiri katika maeneo yao ya taaluma.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa ni muhimu pia kwa vyuo hivyo kuingia mikataba ya makubaliano na vyuo vikuu vya nje ili vipate nafasi ya kuwa na programu za kubadilishana wahadhiri na wanafunzi ili kuongeza nafasi za kujifunza utaalamu ambao haupo nchini

“Vyuo Vikuu vyote Duniani vinaendeleza sana wahadhiri wake na vinaendesha programu za kubadilisha uzoefu hasa katika maeneo wanayoona hawana utaalamu nayo, sasa sisi hatupaswi kujifungia ndani tutoke twende duniani tukajifunze utaalamu na ujuzi zaidi” amesisitiza Prof. Mkenda

Waziri huyo ameongeza kuwa ili kuvutia wahadhiri kutoka nje ni lazima kuwe na mazingira mazuri ambayo yatawawezesha kuishi na kufanya kazi vizuri. Amevitaka Vyuo kuendelea kuboresha mazingira ili kuwa na miundombinu inayokidhi matakwa ya ufunddishaji na ujifunzaji.

“Kuna watu wanadhani uzalendo ni kwamba ajira wasipewe wageni, vyuo vikuu vyote duniani vinaajiri watu wenye uwezo kutoka popote duniani, na sisi tunapaswa kuhakikisha tunatafuta walimu wenye ujuzi ambao hatuna wala tusiogope kuleta watu kutoka nje” ameongeza Prof. Mkenda

Kuhusu kampasi 14 zinazojengwa katika mikoa mbalimbali nchini Mkenda amevitaka vyuo vinavyotekeleza ujenzi huo kuhakikisha unakwenda sambamba na uandaaji wa wahadhiri watakaotumika katika kampasi hizo zitakapokamilika na kudahili wanafunzi.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Prof. Evaristo Liwa amesema kampasi hiyo katika miaka 10 itakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 1090 na itatoa programu 30 za Stashahada na shahada. Aidha amesema Kampasi hiyo itatoa mafunzo kwa kiasi kikubwa yanayoendana na uhitaji na shughuli za kiuchumi za eneo hilo.

Kuhusu kuendeleza wahadhiri Prof. Liwa amesema Chuo chake tayari kimeshapeleka watumishi 10 kwa ufadhili wa mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) masomoni ambapo baadhi wamekwenda Uingereza, Afrika ya Kusini na Nelson Mandela na kwamba wataendelea kupeleka walimu nje kwa ajili ya kujiendeleza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post