WAZIRI MCHENGERWA AZINDUA KAMATI YA USHAURI YA UGAWAJI WA VITALU VYA UWINDAJI, AITAKA IZINGATIE WELEDI,UZALENDO.


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amezindua Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii nchini na kuitaka kurekebisha kasoro zote zilizojitokeza siku za nyuma pia ugawaji ufanyike kwa uwazi ili kuendana na wakati wa sasa hatimaye tasnia hiyo ichangie kwa kiwango stahiki kwenye uchumi wa taifa.

Akisoma hotuba yake wakati wa uzinduzi leo Julai 11, 2023 jijini Arusha, Waziri Mchengerwa amesema ameiunda kamati hiyo kwa mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa kifungu cha 38 (1) na (2) ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori sura ya 283 huku akisisitiza kwamba Kamati hiyo inatakiwa kuboresha changamoto zote ili tasnia ijiendeshe kibiashara na kupunguza urasimu na mikinzano isiyokuwa na tija kwa Taifa.

“Ni imani yangu kwamba, kwa kuzingatia ushauri utakaotolewa na Kamati hii tasnia ya Uwindaji wa Kitalii itazidi kuimarika na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya Nchi. Pia Kamati itasaidia kuhakikisha vitalu vyote vinapata wawekezaji ili kuongezea mapato ya Serikali ikiwa ni pamoja na vitalu 43 ambavyo kwa sasa vipo wazi.” Amesisistiza, Mhe. Mchengerwa

Aidha, amesema anatarajia Kamati hiyo itafanya kazi kwa ufanisi na weledi katika utendaji kwa kuzingatia kuwa imesheheni wataalamu kutoka katika nyanja mbalimbali.

Amefafanua kuwa uwindaji wa kitalii unachangia katika pato la Taifa hususani fedha za kigeni na kwamba kwa wastani, Serikali inakusanya takriban shilingi Bilioni 30 kwa mwaka kutokana na Uwindaji wa huo na unachangia ajira za rasmi na zisizo rasmi kwa jamii.

Amesema kiasi hicho ni kidogo ukilinganisha na utajiri wa raslimali za wanyamapori hapa nchini ambapo ameitaka Kamati hiyo kufanya kazi na kujiwekea malengo makubwa zaidi.

Aidha, ameitaka Kamati hiyo kuzitambua changamoto zinazokabili tasnia hiyo ili kuja na mikakati ambayo itasaidia kuboresha sekta hiyo.

Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na mabadiliko ya Sera na Sheria za Mataifa yanayoleta watalii wengi wa uwindaji, mabadiliko ya tabia nchi,uvamizi wa mifugo katika vitalu vya uwindaji wa kitalii hivyo kuathiri ustawi wa tasnia hii, na kampeni za wapingaji wa uwindaji wa kitalii ambazo kwa kiasi kikubwa zimeingilia maamuzi ya Mkataba wa Kimataifa unaosimamia Biashara ya Wanyamapori na Mimea iliyopo Hatarini kutoweka (CITES).

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu Profesa Jafary Kideghesho, amemhakikishia Waziri Mchengerwa kuwa Kamati yake itafanya kazi kwa weledi ili kufikia maono na Serikali ya kutaka tasnia hiyo kuchangia katia uchumi.

Naye Katibu wa Kamati hiyo ambaye pia ni Kamishna wa Mamlaka ya Wanyamapori nchini (TAWA) Mabula Nyanda amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa kuiunda Kamati hiyo ambapo amesema itasaidia kuboresha tasnia hiyo kwa kuwa imejumuisha wataalaam waliobobea katika tasnia hiyo.

Mara baada ya uzinduzi huo waziri Mchengerwa ametoa nyaraka na miongozo mbalimbali kwa wajumbe wote ikiwa ni namna ya kuwakabidhi nyenzo kwa ajili ya utekelezaji wa kazi zao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post