MLOGANZILA YAZINDUA DUKA LA DAWA LA JAMII


*************

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imezindua duka la dawa la jamii kwa lengo la kuwasaidia wagonjwa na watu mbalimbali kupata dawa ambazo hazipatikani katika maduka ya dawa yaliyopo ndani ya hospitali kwa utaratibu wa kawaida hivyo kupaswa kununua.

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema uamuzi wa kufungua duka hilo utawaondolea usumbufu wananchi wa kwenda umbali mrefu kutafuta dawa na mahitaji mengine muhimu kwakuwa sasa yatakuwa yanapatikana katika duka lililopo ndani ya hospitali.

“Kimsingi lengo letu ni kuendelea kuboresha huduma, katika duka la dawa la jamii kutakuwa na dawa mbalimbali ikiwemo zile ambazo wagonjwa huandikiwa na daktari lakini katika utaratibu wetu wa kawaida hazipatikani katika maduka yetu ya kutolea huduma, pia naomba niwahakikishie kuwa zile dawa ambazo wagonjwa wanatakiwa kupata katika utaratibu wetu wa kawaida ikiwemo kulipia au kutumia bima zitapatikana katika maduka yetu ya ndani” amebainisha Prof. Janabi

Prof. Janabi ameongeza kuwa uongozi utaendelea kuliwezesha duka hilo kimtaji ili liweze kukidhi mahitaji ya wateja wake na kusisitiza kwamba hakuna mgonjwa atakayekosa dawa kwa kuwa itakuwa wajibu wao kuwatafutia dawa kwa lengo la kuhakikisha kuwa wagonjwa wanapata dawa sahihi kwa tiba sahihi.

Duka la dawa la jamii pia litakuwa na bidhaa nyingine mbalimbali ikiwemo dawa za meno,sabuni na daipa , mahitaji haya huhitajika kwa kiasi kikubwa na wananchi wengi wanaopata huduma katika hospitali hii .

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila ina zaidi ya maduka kumi ya dawa katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma ambayo yanawahudumia wagonjwa wa nje na wanaolazwa ambayo yana wataalamu wenye weledi wa kutosha. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post