KATIBU MKUU CCM ATOA MSIMAMO UWEKEZAJI BANDARI DAR ES SALAAM*****************

-Aseema ni mpango ulioko katika Ilani ya Uchaguzi, hivyo Wana CCM wasirudi nyuma

-Asisitiza hatafunga breki wala kuyumbishwa na yoyote katika uwekezaji

-Aiagiza Serikali kuharakisha mchakato wake ili wananchi waone tija yake


Na Mwandishi Wetu ,Mbeya

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Daniel Chongolo amesema ajenda ya uboreshaji na uwekezaji wa bandari ya Dar es salaam liko kwenye Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Chama hicho, hivyo ni mkakati wa Chama na Serikali isirudi nyuma katika kutekeleza uwekezaji huo.

Amesema mpango wa kuboresha bandari ya Dar es Salaam sio wa mtu yoyote bali ni mpango wa CCM , hivyo wana CCM wasikubali kuyumbishwa na maneno ya wanaopinga huku akisisitiza kuitaka Serikali kuhakikisha wanaharakisha mchakato wa uwekezaji kwenye bandari hiyo ili wananchi waone tija yake.

Chongolo ameyasema hayo kwenye mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Ruanda Nzovwe,jijin Mbeya na kuhudhuriwa na wananchi kutoka maneno mbalimbali sambamba na viongozi wa ngazi mbalimbali.

“Ilani ya uchaguzi imetengenezwa mwaka 2020 imeandikwa na timu ya watalaamu waliandaliwa na Chama Cha Mapinduzi(CCM) kufanya kazi hiyo , kwenye ibara ya 59 ukurasa wa 91 ya Ilani ya uchaguzi , pale mtaona ahadi Chama cha mapinduzi kuboresha utendaji wa bandari zetu nchini.

“Bandari ya Dar es Salaam ni miongoni mwao,wengi wanapiga kelele unajua na wanamuingiza na Mwenyekiti wetu kwenye suala la bandari kwamba ni yeye , ni yeye , ni yeye.Mimi ni mtendaji mkuu wa Chama hiki na ahadi za mwanachama wa CCM inasema nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.

“Sasa ngoja niwaambie mwaka 2020 Rais alikuwa mama Samia ?Aliyeandaa ilani ndio aliiwekea malengo ya kuwezesha ufanisi uongezeke kwenye bandari zetu na moja ni Bandari ya Dar es Salaam

“Lakini mjadala wa uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam umeanza mwaka 2019/2020 kwa mazungumzo yaliyokuwepo hapo toka mwaka 2020, mwaka 2020 alimuweka mwekezaji Mama Samia?Leo tuliahidi baada ya kuahidi tunatekeleza”amesema Chongolo.

Amefafanua akitokea mtu yoyote akawasapoti nje ya Chama Cha Mapinduzi kwenda kwa kasi kwenye utekelezaji wa ahadi zao lazima wawe na mashaka na hicho wanachosapotiwa, mtu yoyote ambaye anatoka nje ya Chama hicho kwenye lolote jema wanalofanya lazima apinge.

“Kwasababu anajua tukifanikiwa kulifanya kwa tija yeye atafanya kazi kubwa ya kutafuta namna ya kudanganya danganya ili apokelewe na kukubalika kwa umma , ndio maana hawalali kwenye suala la bandari na ngoja niwaambie kama bandari ni ahadi ni ya Chama Cha Mapinduzi kwanini tunamuingiza Rais?

“Tunasema unajua mkataba huu ni wa Rais na sisi wana CCM tunaingia , hili jambo la mkataba wa bandari iwe jambo la makubaliano iwe nini jambo hili ni la CCM na sio la mtu, kwasababu iko kwenye Ilani yetu, tuliinadi, tulitekeleza kwanini tunaliacha kwa mtu.

“Sasa kila mmoja nataka aseme suala la bandari ni la CCM , na tukicheka na wanaohangaika kupotosha ,wanaotengeneza uongo na uzushi dhambi itakuwa ya kwetu sisi kwa kutosimama kwenye nafasi yetu , kwasababu hiyo Ilani tunatekeleza mambo mengine na kila siku tunadai.

“Ilani ndio iliyobeba matumaini ya uhakika ya kutatuliwa kwa changamoto za wananchi , na matumaini hayo yapo hai kwasababu wote tunaona utatuzi wa mambo hayo.Jamaa zetu wemepita wametengeneza uongo, wameusukuma kweli kweli ili kupotosha dhamira njema ya uboreshaji wa huduma ya bandari yetu,”amesema Chongolo.

Ameongeza na Serikali wameipa kazi na malengo ya kuhakikisha uboreshaji huo unaleta matokeo chanya kwa haraka wanajadili makubaliano ya nchi na nchi , hakuna mkataba wa uendeshaji, kwa bandari yoyote. Sasa mjadala wote unaopotoshwa ni wa mkataba wa nchi na nchi wa kushirikiana kwenye uwekezaji.

“Hatuna mkataba wa uendeshaji wa bandari yoyote na Serikali kwa sura ambayo CCM tunawoana kama wamepunguza kasi ya kujadili mkataba huu ambao ndio utakuwa na majibu mengi yenye maswali mengi ambayo naulizwa na watu.

“Tuagize Serikali wachakate haraka kwenda kwenye mkataba wa bandari , kwasababu uwekezaji wa bandari Chama Cha Mapinduzi kinaenda kwasababu kinajua tija yake, Serikali ianze kwa haraka kwenda hatua ya pili.

“Haya maneno na siasa ni kazi yetu sisi tuliomba kura tukakubaliwa tukapewa ridhaa ya kuongoza nchi,wasihangaike kujibu, tutajibu sisi kwasababu ndio tuliopewa dhamana ,sisi tutakusanya maoni ya wananchi, tutayachakata , tutakayoyaona yana tija tutapeleka huko ili yatekelezwe na sio vinginevyo.

“Wao wakanyage mwendo, tumechelewa tuko nyuma tunataka matokeo. Ngoja niwaambie kwenye takwimu bandari zote nchini zinaingiza kwa mwaka Sh.bilioni 795.226 , ndio tunazoingiza lakini wao wenyewe wanatumia asilimia 99 ya hizo fedha , yaani bilioni 795 mnaingiza halafu bilioni 791 mnatumia kwenye uendeshaji wa kuingiza hizo fedha

“Yaani pamoja na Serikali kuingiza fedha zote serikali inabakiwa na Sh.bilioni tatu, hivi hata kama mjinga utaacha mambo yaende halafu utafute matokeo, wewe utakuwa na akili timamu ? Lakini lazima tujiulize nani anakula hizi bilioni 795 na wakiambiwa sasa huu mlo tunakata tunatengeneza mfumo utakaoleta tija kwa Serikali watafunga mdogo.

“Sasa kwanini tunakubali kutufunga mdomo kama wao zinazalishwa bilioni 795 sisi tunapata bilioni tatu, bilioni 791 zinarudi kwenye matumizi, hapa kuna genge la watu wana mlo hawako tayari kuona mambo yanabadilika, ndio maana kelele nyingi.

“Na wewe angalia sura za wanaopiga kelele, ukiwaangalia huoni kama wanayoyasema yanatoka moyoni wote kuna mahali wanachota na kuwekewa msuko wa kusema wanayoyasema.CCM tuna akili timamu tuko, imara habari yao wataipata wakati pale tija inapatikana.

“Nataka niwambie wana CCM wenzangu msibabaishwe na msiyumbishwe, ajenda hii ni ya CCM , ajenda hii sio ya mtu, makubaliano haya ni ya CCM na utekelezaji wa Serikali ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi,”amesema Chongolo.

Amesisitiza wasikubali kuyumbishwa hata kidogo kwani baada ya ya miaka mitano kukamilika ikifika mwaka 2025 wataulizwa waliyoahidi wametekeleza kwa kiasi gani.Hivyo wawe na majibu waliyoyafanya na matokeo yake.

“Siwezi kusimama hapa kutete jambo ambalo sioni kama lina tija kwa nchi yangu, kwa taifa langu, sasa kuna watu wanaka kienyeji .kama ajenda sio ya CCM hata aje nani haiwezi kupita, jambo hili ni la CCM ukiona mtu wa CCM anashindwa kulitetea na kulipigania kuwa na mashaka na uana CCM wake.

“Tunayo dhamana na nchi hii, tusimame kwenye nafasi yetu, mambo magumu ndio kipimo cha uwezo wa kiongozi, ukiogopa jambo gumu unatia mashaka, kwenye hili CCM tumeamua, hatuyumbi, hatufungi breki, haturudi nyuma, tunaiagiza Serikali ichakate haraka twende mbele, wasitucheleweshe, wakituchelewesha tutapoteza malengo
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post