WANANCHI KARAGWE WAMSHUKURU RAIS SAMIA KWA MIRADI YA KIMKAKATI...BASHUNGWA ATIA NENO

Na Mariam Kagenda _ Karagwe

Wananchi wa wilaya Karagwe wametoa Salamu za shukrani na Pongezi kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miradi mikubwa ya kimkakati kila sekta iliyojengwa na inayoendelea kutekelezwa ndani ya wilaya Karagwe mkoa Kagera.


Salamu hizo zimetolewa na Wananchi katika nyakati tofauti wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ya kukagua miradi ya maendeleo na kuongea na wananchi katika kata za Bugene, Nyakakika, Igurwa na Kanoni.


Wananchi wamemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuridhia na kutoa shilingi bilioni 70 kwa ajili utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Lwakajunju ambao tayari umeishaanza kutekelezwa.


Aidha, Wamemshukuru Rais samia kwa kutoa shilingi bilioni 4 kujenga shule maalum ya Sayansi wa Wasichana katika eneo la Rwambaizi kata ya Kanoni ambayo ipo katika hatua za Ukamilishaji ili kuanza kupokea wanafunzi kidato cha kwanza hadi kidato cha sita.

Katika Sekta ya Miundombinu, Wamemshukuru kwa Ujenzi wa barabara za lami zitakazofungua uchumi wa wilaya ambazo ni barabara ya Karagwe - Nyaishozi mpaka Benako inayoendelea kujengwa, ujenzi kiwango cha lami barabara za Omugakorongo-Igurwa-Murongo ambayo ipo katika maandalizi ya kuanza utekelezaji.


Kadhalika, Barabara ya Omurushaka-Kaisho-Murongo ambayo ipo katika hatua za mwisho za kusaini mikataba na Kipande korofi cha barabara ya Nyakahanga-Bushangaro eneo la "Kujura Nkeito" kimewekwa lami na eneo korofi la "Bigoro" mkandarasi ataanza kazi ya ujenzi wa kilometa 2 za lami. 

Vile vile, Wameshukuru kwa Ujenzi na ukamilishaji wa Hospitali ya Wilaya Karagwe ambayo inaendelea kutoa huduma pamoja na ujenzi wa kituo cha afya cha Kibona kwa ajili ya tarafa ya Kituntu, ujenzi wa kituo cha afya katika tarafa ya Nyabiyonza utakaoanza katika bajeti ya mwaka huu wa 2023/24. 

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa amewahakikishia Wananchi wa Jimbo la Karagwe kuwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwatumikia kwa jitihada kubwa na unyenyekevu mkubwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post