MKUU WA CHUO CHA MAFUNZO YA UFUGAJI NYUKI TABORA - BTI AWEKA BAYANA MATUNDA YA UJIO WA WATU 10 KUTOKA AFRIKA KUSINI



Mkuu wa Chuo cha Ufugaji Nyuki (BTI) mkoani Tabora, Daudi Semu amesema ujio wa Watu 10 kutoka nchini Afrika Kusini waliokuja nchini kwa lengo la kujifunza ufugaji nyuki unafaida kubwa katika Sekta ya Ufugaji nyuki ikiwemo kubadilishana wanafunzi kuja kujifunza katika eneo hilo.


Akizungumza leo mkoani humo, Semu amesema ugeni huo umejumuisha Wataalam na Wafugaji nyuki utatoa fursa kwa wanafunzi kutoka Tanzania na Afrika Kusini kujifunza kwenye eneo hilo kwa kubadilishana kutoka na kwenda katika nchi hizo mbili.


" Tumeshirikiana nao na tumejifunza na tumewaelezea tunachokifanya chuoni hapa kwenye suala la ufundishaji wanafunzi ikiwemo vifaa vya kufundishia pamoja na mashamba tuliyonayo." amesema Semu.

Aidha, Semu amesema kupitia ujio huo wamejua wao wanafanya nini nchini mwao hasa katika eneo la ufugaji nyuki pamoja na kiwanda cha kuchakatia mazao ya nyuki.


"Wamegundua ubora wetu katika sekta hii, Na katika makubaliano hayo sisi tumepiga hatua na wameahidi kuleta wanafunzi kuja kujifunza mahala hapa ." amesema Semu.

Kwa upande wake Mkulima kutoka mkoa wa Kaskazini Magharibi mwa Afrika Kusini, Sello Nthoesane amesema wamekuja Tanzania kujifunza kwenye eneo la ufugaji nyuki na kuona namna wanaweza kushirikiana na Tanzania kwenye eneo hilo.


"Ni uzoefu mkubwa ambao tumeupata tunaona mikakati na Sera iliyopo ya ufugaji nyuki, hakika wanaitekeleza vizuri. Tunaangalia namna ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuweza kusonga mbele."


Sambamba na hayo, Awali kabla ya kutembelea Chuo cha Ufugaji Nyuki (BTI), wageni hao walipatiwa mafunzo ya namna bora ya kutunza na kuchakata mazao ya Nyuki kutoka kwa Meneja wa Mradi wa kuongeza thamani ya Mnyororo wa Thamani wa Ufugaji Nyuki (BEVAC), Martin Lackson Mgallah pamoja na Mratibu wa Kitaifa wa Programu ya Mradi huo, Magdalena Raymond Muya.


Ugeni huo umekuja hapa nchini kwa ajili ya kufanya ziara yenye lengo la kujifunza kuhusu ufugaji nyuki hasa kwenye uzalishaji wa mazao ya nyuki, hifadhi za nyuki, usimamizi wa mazao ya nyuki na namna ya kudhibiti wadudu wasumbufu kwenye ufugaji nyuki.


Aidha, Katika ziara hiyo Wageni wametembea kujionea Vikundi mbalimbali ikiwemo kikundi cha Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) pamoja na Kikundi cha Miombo Beekeepers Group ambao wote wanapatiwa elimu ya ufugaji nyuki pamoja na vifaa vya kuchakatia mazao ya nyuki kupitia Manispaa ya Halmashauri ya Tabora, Mradi wa BEVAC pamoja na Mfuko wa Misitu TaFF

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post