AWESO AZITAKA JUMUIYA ZA WATUMIAJI MAJI NCHINI ZATAKIWA KUSIMAMIA VIZURI MIRADI YA MAJI

Jumuiya za watumiaji maji nchini zimetakiwa kuhakikisha zinasimamia vizuri miradi ya maji ili ziweze kutatua changamoto za maji kwa wananchi na kupata maji safi na salama.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maji Jumaa Aweso wakati wa ziara yake katika wilaya ya Biharamulo ambapo atakuwa na ziara ya siku nne katika mkoa wa Kagera


Waziri Aweso amesema kuwa kumekuwa na kasumba kwa baadhi ya maeneo kamati ambazo zimeundwa kwa ajili ya kusimamia miradi ya maji zimekuwa za kugawana fedha za maji jambo ambalo usababisha miradi ya maji kuharibika na viongozi kugombana wao kwa wao.

Amesema wizara ya maji haitoruhusu wala kumuonea haya mtu yoyote yule anayechezea fedha za miradi ya maji kwani iko tayari kumuwajibisha atakayechezea fedha hizo kwa sababu serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina nia njema ya kumtua mama ndoo kichwani .


Kwa upande wake kaimu Meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini wilaya ya Biharamulo Injinia Lucas Matina wakati akisoma taarifa ya huduma ya maji wilayani humo amesema kuwa mji wa Biharamulo unakadiriwa kuwa na watu takribani 27,432 ambapo kiasi cha maji kinachohitajika kwa siku ili kukidhi mahitaji ni mita za ujazo 1920 kwa siku.

Ameongeza kuwa maji yanayozalishwa kwa siku ni mita za ujazo 1440 ambapo mamlaka hiyo inategemea vyanzo vikuu vitatu ambavyo ni Ruziba, Runyinya na Kagango ambapo mamlaka hiyo inayo mipango ya baadae ya uboreshaji wa huduma ya maji ikiwa ni pamoja na kutoa elimu na kuhamasisha wananchi waishio kando ya vyanzo vya maji kuhusu utunzaji wa vyanzo hivyo


Aidha katika ziara hiyo Mhe. Jumaa Aweso amezindua ujenzi wa tenki la maji mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Biharamulo Mjini ambalo limegharimu kiasi cha shilingi milioni 343,053,790 na limejengwa kwa miezi 6


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments