GGML YATOA MSAADA WA MADAWATI 8,823 MKOANI GEITA


Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong (kulia) akimkabidhi Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigela baadhi ya madawati hayo. Kushoto kwa mkuu huyo wa mkoa ni Mkuu wa wilaya ya Geita, Cornel Maghembe.
Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong, Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigela baadhi ya viongozi wengine wa mkoa huo, wakiwa wamekaa katika madawati hayo pamoja na wanafunzi mkoa huo kama ishara ya furaha ya makabidhiano ya madawati kwa shule mbalimbali za Geita.
Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano ya madawati kwa shule mbalimbali za Geita.

NA MWANDISHI WETU

KATIKA kutimiza dhamira ya kuimarisha sekta ya elimu na kuwezesha mazingira ya utoaji elimu nchini kuwa ya usawa, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetoa msaada wa madawati 8,823 kwa shule mbalimbali za Geita ili kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia kwa wanafunzi wa mkoa huo.

 

Katika hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika juzi Mjini Geita kwa ushirikiano na mamlaka za serikali za mitaa kupitia mpango wa GGML wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, aliishukuru kampuni hiyo kwa kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka.

 

Alisema kadiri shule nyingi zinavyoendelea kujengwa ndivyo hitaji la madawati linavyozidi kuonekana jambo ambalo GGML inajitahidi kutatua changamoto hiyo.

 

Shigella alipongeza GGML kwa kuwa na mipango ya muda mrefu ya kuinua sekta ya elimu mkoani Geita na Tanzania nzima kwa ujumla.

 

"Ni furaha yangu kwamba tangu GGML ianze shughuli za uchimbaji hapa mkoani Geita, imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Serikali kutekeleza miradi kadhaa ya elimu, hasa ujenzi wa madarasa na shule".

 

Mkuu huyo wa mkoa alikiri kuwepo kwa uhaba wa madawati katika shule mbalimbali hivyo kuwaomba wadau wengine mkoani humo kufuata nyayo za GGML katika kuboresha mazingira ya kujisomea kwa wanafunzi.

 

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong, alisema ni muhimu kuboresha mazingira ya utoaji elimu nchini ili kufikia lengo namba 4 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.

 

"Kutoa elimu bora kwa wote ni msingi wa kujenga dunia yenye amani na ustawi. Elimu huwapa watu maarifa na ujuzi wanaohitaji ili kuwa na afya njema, kupata ajira. GGML inafurahi kuboresha maisha ya Watanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu," alisema.

 

Akielezea malengo ya GGML katika kuboresha maisha ya Watanzania hususani kupitia uboreshaji wa sekta ya elimu, Strong alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo mwaka wa 2000, GGML imeendelea kuwekeza katika nyanja mbalimbali zinazoboresha maisha ya jamii nzima ya Geita na Tanzania kwa ujumla.

 

Alisema GGML imewekeza kwa kuzingatia masuala muhimu kama vile afya, elimu, maji, barabara na miradi ya kuzalisha kipato cha kaya na kukuza uchumi wa Taifa.

 

"GGML imewekeza katika utekelezaji wa miradi endelevu ambayo inainufaisha jamii inayouzunguka mgodi. Kwa hiyo mchango huu wa madawati unadhihirisha jukumu la GGML kama mwananchi anayehitaji elimu bora kubadilisha maisha yake," alisema na kuongeza;

 

"Juhudi za GGML kujitolea kutekeleza miradi mbalimbali zinaendelea kuacha alama isiyofutika na kusaidia kuboresha maisha ya jamii kupitia uwepo wa kampuni hii mkoani Geita."


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post