TGNP YAENDESHA MAFUNZO KWA WABUNGE KUHUSU UMUHIMU WA KUANDAA BAJETI ZENYE MRENGO WA KIJINSIA

Mchambuzi wa sera na kanuni za Bunge, Deus Kibamba akizungumza Leo Juni 13,2023 Jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha mada kwenye mafunzo kwa wabunge kuhusu umuhimu wa bajeti kuwa na mlengo wa kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum akizungumza Leo Juni 13,2023 Jijini Dodoma katika mafunzo kwa wabunge kuhusu umuhimu wa bajeti kuwa na mlengo wa kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP.


Na Okuly Julius-Dodoma

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umewataka wabunge kuisimamia serikali kuandaa bajeti zenye mlengo wa kijinsia zitakazo saidia kujibu kero za kila kundi nchini kwa maendeleo endelevu.


Mchambuzi wa sera na kanuni za Bunge, Deus Kibamba ameyasema hayo Leo Juni 13,2023 Jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha mada kwenye mafunzo kwa wabunge kuhusu umuhimu wa bajeti kuwa na mlengo wa kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP.


Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuboresha uwezo wa kupenyeza masuala ya usawa wa kijinsi kwenye michakato ya kibajeti bungeni.


“Lengo la mafunzo kwa wabunge hawa ni kuwawezesha kuwa na uwezo wa kupenyeza masuala ya kijinsia kwenye michakato ya kibajeti kuanzia ngazi za chini kwakuwa wabunge pia ni madiwani wataweza kupenyeza ajenda hii hadi katika ngazi za chini”amesema Kibamba


Pia, Kibamba amesema ili kufanikisha ajenda ya bajeti zenye usawa wa kijinsia wanawake wanapaswa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali ili kusimamia michakato hiyo kwa ukamilifu.


“Mwakani tunakwenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wanawake wanapaswa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali ili kusimamia michakati ya bajeti zenye mlengo wa kijinsia.


“Hatua kubwa zimepigwa kwenye mambo mbalimbali nchini kwenye masuala ya kijinsia leo hii sisi kama taifa hatushangai kuona waziri kuwa mwanamke au spika kuwa mwanamke lakini bado yapo mambo madogo ya kufanyia kazi lakini katika ngazi za chini tatizo bado kubwa sana kwenye vijiji na mitaa takwimu zinaonyesha kuwa kwenye ngazi za serikali za mitaa wanawake viongozi hawazidi asilimia tatu”amesema Kibamba


Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Simiyu Leah Komanya, amesema wabunge wanao wajibu wa kuisisitiza serikali pamoja na jitihada za kujenga majengo kwa ajili ya vituo vya afya pia kuwepo na vifaa vya uhakika vya wanawake kujifungulia.


“Serikali pia itekeleze ujenzi wa kiwanda cha vifaa tiba ili kuondoa changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili wanawake na wasichana ikiwemo upatikanaji wa taulo za kike zinazochangia kuwakosesha masomo wasichana”amesema Komanya


Mbunge wa Mikumi Dennis Londo, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa wabunge na yanapaswa kutolewa mapema ili waweze kuishauri serikali kabla ya kusomwa kwa bajeti kuu.


“Mpango wa bajeti unaletwa katika Bunge la mwezi Novemba hivyo mnatakiwa kabla ya wakati huo mchambue mapendekezo yenu ili sisi tunapochangia bungeni tunakuwa na uhakika na kile tunacho kisema ili kuwasaidia wanachi kwenye vipaumbele vyao”amesema Londo


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum amesema wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kuwa michakato ya bajeti inakuwa na mlengo wa kijinsia kwa kuwa maendeleo ya taifa lolote yanapaswa kujali usawa wa kijinsia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post