TBS KANDA YA ZIWA YATOA MAFUNZO KWA WAFANYABIASHARA WA VIFAA VYA UJENZI MWANZA

 
Wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa za ujenzi jijini Mwanza wakiwa kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na TBS yaliyolenga kuwawezesha kuagiza a kuzalisha bidhaa zenye ubora.

************

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Ziwa, limetoa mafunzo kwa wafanyabiashara waagizaji na wazalishaji wa vifaa vya ujenzi jijini Mwanza ili kuwajengea uelewa kuhusu Sheria, Kanuni na Miongozo ya udhibiti ubora wa vifaa hivyo.

Akifungua mafunzo Juni 26, 2023, Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Emil Kasagala aliwataka wafanyabiashara hao kuwa wazalendo kwa kuagiza na kuzalisha vifaa vyenye ubora vinazokidhi viwango vya TBS kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Kasagala alisema lengo la Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona vifaa vinazoingizwa sokoni vinakidhi ubora wa kimataifa ili kuleta tija kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi pamoja na ile ya kimkakati ikiwemo daraja la JP Magufuli lililopo eneo la Kigongo- Busisi pamoja na meli mpya ya MV. Mwanza.

“Vifaa vya ujenzi visivyo na ubora ikiwemo mabati, misumari na nondo vinaweza kusababisha hasara kwa wananchi na taifa hivyo tunawasihi kutanguliza uzalendo kwa kuagiza na kuzalisha vifaa vyenye ubora” alisema Kasagala na kuongeza;

“Tutimize wajibu wetu kwa kuhakikisha vifaa mnavyoagiza nje ya nchi ama kuzalisha wenyewe hapa nchini vinakuwa na bora na salama. Majengo ya zamani yalidumu kwa sababu ya ubora wa vifaa vya ujenzi hivyo tunataka kuona hata sasa miradi tunayotekeleza inadumu zaidi ya miaka 100 ijayo” alisema Kasagala.

Naye Afisa Usalama wa Chakula TBS Kanda ya Ziwa, Nuru Mwasulama alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa kutoa elimu kwa umma kuhusu ubora wa bidhaa na vifaa mbalimbali kulingana na Sheria na Viwango vilivyowekwa na TBS hatua itakayosaidia kuondoa sokoni bidhaa na vifaa vilivyo chini ya kiwango.

“Tunatamani kuona watanzania wana uelewa wa kuhoji mambo ya msingi kuhusu ubora wa bidhaa na vifaa vilivyothibitishwa na TBS ndiyo maana tunaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali. Lengo letu si kukamata tu bidhaa na vifaa visivyokidhi viwango bali pia kutoa elimu kwa wafanyabishara na wananchi ili ziepuka” alisema Mwasulama.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Meneja wa kampuni ya uzalishaji vifaa vya ujenzi ya TAISHAN Kanda ya Ziwa, Issaac Maro na Salma Mwichande kutoka kampuni ya ujenzi ya DF Mistry walishukuru TBS kuwajengea uelewa kuhusu viwango vinavyotakiwa na kuahidi kuendelea kuagiza, kuzalisha na kutumia vifaa vyenye ubora.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Emil Kasagala akifungua mafunzo kwa wafanyabiashara na wazalishai wa vifaa vya ujenzi jijini Mwanza.
Afisa Usalama wa Chakula TBS Kanda ya Ziwa, Nuru Mwasulama akizungumza kwenye warsha ya kuwajengea uelewa wafanyabiashara wanaoagiza na kuzalishaji bidhaa za ujenzi jijini Mwanza.

Wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa za ujenzi jijini Mwanza wakiwa kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na TBS yaliyolenga kuwawezesha kuagiza a kuzalisha bidhaa zenye ubora.

Afisa Viwango TBS akiwasilisha mada kuhusu Sheria, Miongozo na Kanuni zinazotumika kudhibiti bidhaa wakati wa warsha ya kuwajengea uelewa wafanyabiashara wazalishaji na waagizaji wa bidhaa za ujenzi jijini Mwanza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post