SERIKALI YAZINDUA MIKATABA YA HUDUMA KWA WATEJA

 

Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais,menejmenti ya utumishi wa Umma na utawala bora George Simbachawene akizungumza na waandishi wa habari kwenye uzinduzi wa mikataba ya huduma Kwa wateja ya Taasisi za Umma.

 Na Dotto Kwilasa,Dodoma.

Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora,imezindua mikataba ya huduma kwa wateja kwa Taasisi za umma huku ikitoa maagizo kwa taasisi zote za umma nchini kuwa na mikataba ya huduma kwa wateja iliyo hai .

Waziri mwenye dhamana hiyo George Simbachawene ameeleza hayo leo Juni 23,2023,jijini Dodoma katika uzinduzi wa mikataba hiyo na kuzielekeza Taasisi za umma kujenga uelewa kwa wateja kuhusu mikataba hiyo.

Amesema,matumizi ya mikataba hiyo yataleta mafanikio kadhaa ikiwemo kuwezesha watumishi kuongeza uwajibikaji na nidhamu kazini ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa uwazi na weledi.

",Tumezindua mikataba ya huduma Kwa wateja,ni matarajio makubwa kwetu kuwa itasaidia kuchochea ari ya kufanya kazi kwa bidii, vile vile itaongeza watumishi  wa umma kuwa na utamaduni wa utendaji kazi unaojali matokeo na tija kwa wakati na kwa maslahi mapana ya watanzania,"anasisitiza 

Waziri huyo pia amesema pamoja na mafaniko hayo yapo mapungufu ambayo yamejitokeza ikiwemo kukosekana na kutohuishwa kwa mikataba  ya huduma kwa wateja,uelewa mdogo wa  kuhusu mikataba hiyo na usimamizi usioridhisha. .

Simbachawene amesema,"Naagiza taasisi zote za umma ziwe na mikataba ya huduma kwa wateja iliyo hai pamoja na kujenga uelewa kwa wateja kuhusu mikataba hiyo ili kusiwe na malalamiko yoyote,"anasema.

Pamoja na hayo ameeleza,"Ni Matumaini yangu kuwa  kuimarika kwa matumizi  ya mifumo ya utendaji kazi serikalini  hususani matumizi ya mikataba  ya huduma kwa wateja italeta mageuzi makubwa ya utendaji  unaojali matokeo na kutakuwa na ungezeko  la uwajibikaji, ufanisi katika matumizi  ya rasilimali nyingine katika sekta za umma,"anasisitiza.

Amesema serikali ina jukumu la kuwezesha wananchi kupata huduma bora  ikiwa ni pamoja na elimu,afya,maji ,mawasiliano  ambapo ili kufanikisha jambo hilo Serikali ina sanifu na kujenga mifumo.

Naye Katibu Mkuu, Ofisi Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Juma Mkomi amesema taasisi za umma zimekuwa zikiadhimisha wiki ya utumishi wa umma ambayo hufanyika kila mwaka kuanzia Juni 16 hadi 23 kwa lengo la kutambua mchango wa watumishi wa umma katika maendeleo ya nchi zao.

Amefafanua kuwa ni azma ya Serikali kuhakikisha kila taasisi inakuwa na mkataba wa huduma kwa wateja na kuutekeleza ipasavyo  ili kuboresha utoaji wa huduma kwa umma na kwamba  katika kufanikisha hilo,ofisi yake ilitoa maelekezo kwa taasisi zote za umma kuhuisha mikataba hiyo na kuhakikisha zinakuwa hai.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Sospeter Mtwale , ameeleza kuwa pamoja na juhudi zilizopo bado mikataba ya watumishi wa umma katika ofisi za Serikali ya mitaa hazijazingatiwa katika ngazi ya mikoa na mitaa hivyo Serikali inaendelea kuhamasisha kila Taasisi kufuata utaratibu.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post