HALMASHAURI YA MULEBA IMEENDELEA KUPATA HATI SAFI MIAKA 5 MFULULIZO



 Katibu Tawala mkoa wa Kagera Toba Ngunvila 
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Muleba Justus Magongo
Madiwani wakiwa ukumbini.

Na Mwandishi wetu - MALUNDE 1 BLOG

Halmashauri ya wilaya ya Muleba mkoani Kagera imeagizwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa ukusanyaji wa mapato na kuibua vyanzo vipya vya mapato jambo ambalo litasaidia halmashauri hiyo kuendelea kupata hati safi.


Agizo hilo limetolewa na Katibu Tawala mkoa wa Kagera Toba Ngunvila wakati akisoma taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ( CAG) akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Kagera katika kikao maalum cha kujadili taarifa hiyo ambapo halmashauri ya wilaya ya Muleba imepata hati safi katika kipindi cha miaka 5 mfululizo.
.

Bwana Ngunvila amesema kuwa agizo hilo la serikali linatakiwa kuendelea kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha 2022/2023 na kuhakikisha juhudi za makusudi zinafanyika ili mapato yote ya halmashauri yakusanywe kwa njia ya kielektroniki na sio vinginevyo ambapo madiwani wanatakiwa kusimamia swala hilo .


Kikao hicho ni mwendelezo wa utekelezaji wa Agizo la Mhe.  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akipokea taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kwa mwaka 2021/2022 ambapo alielekeza kila Taasisi ifanyie kazi taarifa hizo na kuhakikisha hoja husika zinafungwa.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Muleba Justus Magongo amesema kuwa katika mafanikio ya halmashauri hiyo kupata hati safi ni kutokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina ya watumishi wa halmashauri hiyo na madiwani wa kata 43 ambapo ameaidi kuwa halmashauri hiyo itaendelea kufanya vizuri hasa kwa kusimamia mapato kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo.


Aidha ameishukuru ofisi ya mkuu wa mkoa na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Muleba kwa ushirikiano wanaowapatia ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa halmashauri hiyo kuendelea kufanya vizuri.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post