WAZIRI MCHENGERWA ATEKELEZA AGIZO LA WAZIRI MKUU, AFIKA ENEO LA TUKIO, ATOA POLE NA MAAGIZO MAZITO KWA WATENDAJI.



Na John Mapepele

Agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alilolitoa jana bungeni la kutaka Waziri wa Maliasili na Utalii na Watendaji wa Wizara hiyo kufika mara moja kijiji cha Mwanavala wilayani Mbarali wakishirikiana na Uongozi wa Mkoa wa Mbeya kutatua migogoro baina ya Hifadhi ya Ruaha na wananchi hao limekamilika leo Mei12,2023 baada ya kufika.

Akiongea kwenye kikao na wananchi hao leo mei 12, 2023 amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuwachukulia hatua za kinidhamu maafisa wote wa Serikali walioshiriki kwenye migogoro huo.
Hata hivyo amewaomba wananchi kuzingatia sheria ambapo amewataka kutovamia maeneo ya makazi ambapo katika mgogoro huo baadhi ya wananchi walikutwa kilomita kumi ndani ya Hifadhi ndipo walipoanza kutolewa kwa nguvu na wahifadhi.

Mhe. Mchengerwa ametoa mkono wa pole wa shilingi milioni moja kwa wananchi watano kila moja kama kifuta machozi kutokana na ugomvi wa wahifadhi na wananchi hao. Hata hivyo hakuna tukio lolote la kifo.

Amefafanua kuwa tatizo la mipaka katika Hifadhi hiyo linakwenda kumalizika ambapo amesema jumatatu anasaini GN mpya ya mpaka wa eneo hilo.
Hata hivyo imethibitika kuwa madai ya kwamba ng'ombe 250 walishikiliwa siyo ya kweli kwa kuwa wananchi wote katika mkutano wamekubali kuwa hakuna ng'ombe hata moja aliyeshikiliwa na Hifadhi

Aidha amesema mipaka ya Hifadhi hiyo iliwekwa mwaka 1910 wakati Hifadhi hiyo ikijulikana kama Saba Game Reserve na mwaka 1946 ikijulikana kama Hifadhi ya Rungwe na hatimaye mwaka 1964 kama Hifadhi ya Ruaha hadi sasa.

Ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona kuwa kero zote katika maeneo ya Hifadhi zinatatuliwa kwa amani na upendo.

"Ibara ya 68 ya CCM inasisitiza uhifadhi wa raslimali hivyo sisi sote tunapaswa kushirikiana kwa pamoja tuhifadhi kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye" ameongeza Mhe. Mchengerwa
Katika kikao hicho, bwana Ngalao Laini ameiomba Serikali kuangalia namna bora ya kuwahamisha wananchi na kuwatengea maeneo bora ya makazi pindi inapoamuliwa kuwaondoa katika Hifadhi.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye pia aliambatana katika ziara hiyo na Kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa, na wilaya ya Mabarali na viongozi wa CCM wa wilaya hiyo aliwaambia wananchi katika mkutano huo kuwa Serikali itahakikisha kuwa wananchi wote wanatendewa haki ikiwa ni pamoja na kufanya tathimini za makazi na kuwalipa fidia stahiki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post