VIJANA 148 WAENDA DENMARK NA SAUDIA ARABIA KUFANYA KAZI


Na Mwandishi Wetu

VIJANA 148 wameondoka nchini kwenda Denmark na Saudi Arabia kwa ajili ya kufanya kazi pamoja na mafunzo ya uzoefu wa kazi (internship) yanayoratibiwa na Kitengo cha Huduma za Ajira(TaESA) kilichopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Akizungumza na kundi la mwisho la vijana hao katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Mei 18, 2023, Mkurugenzi wa Kitengo hicho, Joseph Nganga, amesema vijana hao wameondoka Mei 17 na 18, 2023 ambapo kati yao 68 wameunganishwa na Wakala wa ajira Bravo Job Centre kwenda nchini Saudi Arabia kufanya kazi kwenye kampuni ya ufugaji na usindikaji wa bidhaa za mifugo ya Almarai.

Amesema vijana wengine 80 wameunganishwa na Wakala wa Ajira SUGECO kwenda nchini Denmark kufanya kazi kwa mpango wa mafunzo ya uzoefu wa kazi kwenye kampuni mbalimbali zinazojihusisha na kilimo na ufugaji.

Mkurugenzi Nganga amewataka vijana hao kufanya kazi kwa bidi, kuwa wabunifu pamoja na kuzingatia maadili ya kazi ili waendelee kuaminiwa pamoja na kufungua fursa zaidi kwa watanzania kuajirika katika kampuni hizo na nchi zingine.

Amepongeza Wakala wa Bravo Job Centre pamoja na SUGECO kwa juhudi wanazozifanya kuwezesha vijana kupata fursa za ajira na mafunzo ya uzoefu wa kazi kwenye nchi mbalimbali duniani.

“Wito wangu kwa Wakala wote wa ajira waliosajiliwa kuongeza juhudi katika kuibua fursa za ajira na kuwaunganisha watanzania na kazi za staha kwenye nchi mbalimbali na kwa vijana wenye nia na shauku ya kufanya kazi nje ya nchi wazingatie utaratibu rasmi zilizowekwa na serikali,”amesema.

Amesisitiza serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kuwezesha watanzania kunufaika na fursa hizo na kuwajengea uwezo vijana kuwa na ujuzi na sifa stahiki zinazohitajika pamoja na kufanya majadiliano yenye lengo la kusaini hati za mashirikiano na nchi za kimkakati ili kufungua fursa zaidi za ajira kwa watanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments