MBUNGE CHIKOTA AHOJI MIKOPO KWA WAKULIMA WA KOROSHO




MBUNGE wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota ,akiuliza maswali bungeni leo Mei 2023 katika Mikutano inayoendelea bungeni jijini Dodoma

 Na Mwandishi Wetu, DODOMA 

MBUNGE wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota ametaka serikali kuweka mpango wa kuhakikisha wakulima wa korosho wanapata mikopo ili kugharamia kilimo cha korosho.

 Akiuliza maswali bungeni leo, Chikota ametaka serikali itoe tamko kwa taasisi za fedha ambazo zimeacha kuwapatia mikopo kwa wakulima nchini baada serikali kuanza kutoa ruzuku ya pembejeo. 

Aidha, amesema baadhi ya kero zinazoyakabili mazao ya kimkakati zingeweza kutatuliwa na mfuko wa maendeleo ya kilimo na kuhoji lini mfuko huo utaanza.

Akijibu swali hayo, Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde, amesema Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) inaratibu uwezeshaji wa wakulima wa korosho kupata mikopo ya kuendeleza zao la korosho ikiwemo pembejeo na utunzaji wa mashamba.

 “Uwezeshwaji huo utafanyika kupitia Vyama Vikuu vya Ushirika kuwawekea dhamana wakulima ili waweze kupata mikopo kutoka katika taasisi za fedha,”amesema.

Vilevile, amesema serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kuwaunganisha wakulima na Taasisi za Fedha ili waweze kupata mikopo yenye riba nafuu kuanzia asilimia tisa kushuka chini. 

Kadhalika amesema serikali pamoja na Tume ya Maendeleo ya Ushirika wamekaa taasisi za kifedha kujadiliana na jambo hilo huku akibainisha baadhi ya kero zilizojitokeza ikiwamo ya urejeshaji wa mikopo hiyo ambayo ilitokana na wakulima wengi kutosajiliwa. 

Amesema kwasasa wakulima wengi wameshasajiliwa na kila mkulima atatambulika shamba lake lilipo, ukubwa wa shamba lake ili kumrahisishia taasisi za fedha namna bora ya kumpatia mkopo mkulima. “Naamini katika hili wakulima wengi watapata mikopo kupitia taasisi za kifedha,”amesema.

Akizungumzia kuhusu mfuko wa maendeleo ya kilimo, Mavunde amesema mfuko huo umeshaanza kufanya kazi na kwamba muda mrefu watapata vyanzo vya kuutunisha ili wakulima wanapopata vikwazo wapate huduma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post