DC BOMBOKO AHIMIZA WAZAZI KUTAMBUA WAJIBU WAO KATIKA KUMLEA MTOTO


Na Dotto Manumbu, Ukerewe

Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe imeadhimisha Siku ya Familia Duniani wilayani hapo kwa kufanya mdaharo uliowahusisha viongozi mbalimbali wa Serikali, Dini, Wananchi na Wanafunzi wa Kidato cha Tano Shule ya Sekondari Bukongo ambapo Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Hassani Bomboko amesisitiza wajibu wa usimamizi wa familia ni kila mmoja ili kuimarisha maadili na upendo kwa familia imara.

Maadhimisho ya Siku ya Familia katika Wilaya ya Ukerewe yakiongozwa na Kauli mbiu ya Mwaka 2023 "Imarisha Maadili na Upendo kwa Familia Imara" yamefanyika leo Jumatatu Mei 15, 2023 ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Hassani Bomboko.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mhe. Bomboko alisema ili kuwa na familia zenye maadili na upendo serikali inapendekeza wanafamilia ikiwahusisha Baba, Mama, Watoto, Ndugu na Jamaa nzima kukaa pamoja ili kujadili mafanikio katika familia, pia kujadili changamoto zilizopo ili kutafuta majibu ya pamoja kwa amani na upendo ili kuendelea kudumisha mshikamano na maelewano ndani ya familia na jamii yote kwa ujumla.

"..madhumuni ya Siku ya Familia Duniani ni kuhamasisha, kuhimiza, kuelimisha na kutanabahisha jamii kuhusu umuhimu wa familia katika jamii kwa nia ya kuchukua hatua zinazopasa ili kuziimarisha na kuziendeleza.."

Mhe. Bomboko amewaasa wananchi na viongozi wa dini kutoa mafundisho mema kwa jamii juu ya masuala kushiriki vyema shughuli za maendeleo katika maeneo yao, kukemea masuala ya ushoga, kupinga masuala ya Uvuvi Haramu, Wazazi (Baba) kufahamu wajibu wao katika kuijenga familia bora na jamii iendelee kudumisha amani katika Wilaya ya Ukerewe.

" ..maadhimisho haya yanatukumbusha wazazi na walezi kutambua wajibu wetu wa msingi juu ya malezi ya watoto na familia hasa kwa akina baba kujua wajibu wao kama wazazi au walezi kwa Watoto katika maeneo makuu 3 ya msingi ambayo ni kumjali mtoto katika maeneo ya msingi, kumlinda mtoto dhidi ya ukatili na kuzungumza na mtoto mara kwa mara ili kufahamu changamoto zinazomkabili na maendeleo yake kwa ujumla”,alisema Mhe. Bomboko

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Emmanuel Sherembi amewasisitiza wananchi wote kutokomeza masuala ya Ukatili wa kijinsia kwa watoto na wazazi kutoa elimu sahihi kwa watoto ili kuondoa tatizo la watoto wa mtaani.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Ukerewe Bi. Eliarusia Nassary amewataka wazazi kujenga msingi bora kwa watoto kwa kuwapeleka Shule na kufuatilia mienendo yao, wazazi kushirikiana katika malezi ya watoto na wazazi wahusike kupinga mila potofu zinazo ikandamiza jamii ili kuwajengea uwezo vijana watakao saidia kuchochea maendeleo katika nchi yao.

Aidha, Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Ukerewe Nasra Msuya amefafanua kuwa suala la Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto wazazi na walezi wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuwalea watoto hao ili kuwa na kizazi bora na imara kwenye familia.

Msuya amesisitiza kuwa wazazi na walezi watenge muda mwingi wa kukaa na watoto wao ili wajadili changamoto na kuzitatua.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya jamii Wilaya ya Ukerewe Wanchoke Chinchibera amehimiza wazazi kuendelea kuboresha maadili ya watoto kwa kuwahusisha katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo Kilimo, Ujasiliamali na Uzalendo kwa nchi yao.

Akitoa maoni yake katika Mdaharo huo Bi. Happy Magesa Mkazi wa Nansio Ukerewe amesema familia nyingi za Kitanzania zinakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mila na desturi zenye kuleta madhara, umaskini uliokithiri, mawasiliano na miundo mbinu mibovu ambapo husababisha hali ya maisha ya watu kuwa duni na tegemezi na hatimaye kutumia muda mwingi wa kufanya kazi bila ya kujali madhara yatakayotokea kwa familia. Madhara haya ni pamoja na watoto kuwa na tabia mbaya kama kuacha shule, kukimbilia mitaani, kutokuwa na maadili na kuiga tamaduni zisizokubalika katika jamii yetu.

"..ni wazi kuwa changamoto hizi zinaweza kushughulikiwa vyema kuanzia ngazi ya familia na ngazi mbalimbali za uongozi, napenda kuwaasa wazazi wenzangu kutenga muda wa kutosha kukaa na familia zao ili kujadili, kushauriana na kutekeleza masuala muhimu ya kuendeleza familia zao kwani familia ndiyo kitovu cha maendeleo.

Tangu tarehe 15 Mei 1989 hadi 15 Mei 2023 ni miaka 34 tangu Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulipoweka Siku ya Kimataifa ya Família.

Umoja wa Mataifa umetenga siku hii kwa ajili ya kutoa fursa ya kuchagiza uelewa wa masuala yanayoathiri familia ikiwemo kijamii kiuchumi na kidemografia.

Kutokana na umuhimu wa familia kama chanzo cha jamii, maadhimisho hayo yanatokana na tamko la Baraza la Umoja wa Mataifa Na. 47/257 la Tarehe 20 Septemba, 1993, linaloidhinisha kuwa na Siku maalum kwa ajili ya familia. 

Tanzania ni moja ya wanachama wa Umoja wa Mataifa hivyo huungana na nchi nyingine kila mwaka kuadhimisha siku hii.

Imeandaliwa Na:
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments