WAPOTEZA UWEZO WA KUONA BAADA YA KUNYWA POMBE HARAMU

Wanaume wawili wanaripotiwa kupoteza uwezo wa kuona baada ya kunywa pombe haramu katika kaunti ya Kirinyaga huku vita dhidi ya mihadarati vikichacha Mlima Kenya.

Kwa mujibu wa kamishna wa kaunti ya Kirinyaga Naiyoma Tobiko, wawili hao ni Julius Munene mwenye umri wa miaka 28 na Joseph Bundi mwenye umri wa miaka 45.

Kamisha Tobiko amewasihi wakaazi kutotumia pombe haramu akisema kuwa ni hatari kwa afya yao na kutoa onyo kali kwa wote wanaoendeleza biashara hiyo.

"Nani amekwambia pombe unayokunywa na dawa za kulevya unazotumia ni nzuri kwa afya ya bindamu? Pamoja na serikali ya kaunti, vita dhidi ya pombe hizo vitaendelea hadi pale ambapo zitafukuwa kabisa kutoka Kirinyaga," Tobiko alimaka.

Gachagua asema pombe imemaliza betri za wanaume Mlima Kenya

Haya yanajiri takriban wiki mbili baada ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kusema kuwa betri za wanaume wa Mlima Kenya zimeisha chaji kwa sababu ya pombe haramu.

"Kwa sababu pombe inamaliza betri zote kwa hii vijana wetu. Betri zote zimeisha na hata ikiekwa chaji haiwezi kufufuka. Kwa hivyo, wanawake wetu wanalia," Gachagua alisema. Mbunge huyo wa zamani wa Mathira alisema kuwa kina mama eneo la Mlima Kenya wanalia kulala pekee yao huku shule zikikosa wanafunzi. "Vijana wetu wameisha. Badala ya kulala kitandani, sasa wanalala kwa sakafu," Gachagua aliongeza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post