BEI YA MAFUTA YASHUKA


******************

Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei mpya za ukomo wa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa huku bei ya bidhaa hizo ikipungua ikilinganishwa na mwezi Machi.

Mabadiliko haya ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia, gharama za usafirishaji na thamani ya shilingi ikilinganisha na dola ya Marekani.

Taarifa iliyotolewa Jumanne Aprili 4,2023 na Mkurungenzi Mkuu wa EWURA, Dk James Mwainyekule imesema kuwa bei hizo zitaanza kutumika kuanzia Jumatano Aprili 5 mwaka huu.

Amesema kwa Aprili 2023, bei za rejareja za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa yaliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimepungua petroli Sh187, dizeli Sh284 na mafuta ya taa Sh169 kwa lita ikilinganishwa na toleo la tarehe Machi 2023.

“Kwa mikoa ya Kaskazini Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, bei za rejareja za Aprili mafuta ya petroli imepungua kwa Sh158, dizeli Sh158 na mafuta ya taa Sh231, ikilinganishwa na toleo la Machi Mosi mwaka huu,” imeleza taarifa hiyo.

Aidha taarifa hiyo ilieleza kuwa kutokana na kuisha kwa mafuta ya taa kwenye matanki ya kuhifadhia yaliyopo Tanga, waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Kaskazini wanashauriwa kuchukua mafuta ya taa kutoka katika bandari ya Dar es Salaam.

“Bei za rejareja za mafuta ya taa katika mikoa hiyo itakuwa kulingana na gharama za kupokelea mafuta ya taa kupitia Bandari ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika,”

Katika Mikoa ya Kusini Mtwara, Lindi, na Ruvuma, bei za rejareja za Aprili 2023 kwa mafuta ya petroli imepungua kwa Sh220, dizeli Sh220 na mafuta ya taa Sh176 iwa lita ikilinganishwa na toleo la Machi Mosi.

“Kwa kuwa hakuna matanki ya kuhifadhia mafuta ya taa katika Bandari ya Mtwara, waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Kusini wanashauriwa kuchukua mafuta ya taa kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam na hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa katika mikoa hiyo itakuwa kulingana na gharama za kupokelea mafuta ya taa,”

Katika taarifa hiyo Dk James alibainisha kuwa tofauti ya bei kutoka sehemu moja kwenda nyingine inatokana na tofauti ya bandari mafuta yanapochukuliwa na gharama ya usafirishaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments