WAZIRI BITEKO ATAKA BAJETI YA 2023/24 KUZINGATIA VIPAUMBELE VYA WIZARAWaziri wa Madini nchini nchini Dkt.D Biteko.


Na Dotto Kwilasa, DODOMA.

SERIKALI kupitia Wizara ya  Madini imewataka Watumishi wa Wizara ya Madini kuhakikisha Bajeti iliyopangwa kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 inazingatia uimarishaji wa ukusanyaji maduhuli ili kufikia lengo la kuchangia asilimia10 kwenye Pato la Taifa.

Waziri Biteko ameyasema hayo Machi 19, 2023, wakati akifungua Mkutano wa baraza la Wafanyakazi Wizara ya Madini ambalo pia lilihudhuriwa na Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya wizara na wawakilishi kutoka Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Makao Makuu.

Aidha, amewataka watumishi na wataalam wa wizara kuweka nguvu katika uendelezaji wa madini ya kimkakati, uendelezaji wa wachimbaji wadogo, uongezaji thamani madini na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara.

"Katibu Mkuu Wizara ya Madini hakikisha unasimamia fedha zinazopatikana kutekeleza majukumu yaliyopangwa kwa kuzingatia vipaumbele vya wizara bila kusahau haki na stahili za watumishi kwa kuwa ustawi wao ndio nguzo katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi,"amesema 

Aidha, Waziri Biteko ametumia fursa hiyo kuwapongeza watumishi wa wizara na kueleza kuwa, pamoja na kuwepo changamoto za kibajeti, hali hiyo haijawazuia kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao. Kufuatia hali hiyo, amewataka kuhakikisha wanatekeleza majukumu kwa tija na kutoa matokeo chanya ambayo yatapelekea kupatiwa fedha za kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali akizungumza katika mkutano huo pamoja na mambo mengine  amesema  kumekuwa na utekelezaji mzuri wa malengo  yaliyowekwa na wizara kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023  ambayo yamepelekea  kuwepo mafanikio kadhaa ikiwemo ongezeko la mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa kwa robo ya Tatu ya Mwaka 2022 (Julai – Septemba 2022) hadi kufikia asilimia 9.7 ikilinganishwa na asilimia 7.9 kwa kipindi kama hicho mwaka 2021

Aidha, ameyataja mafanikio mengine kuwa ni ongezeko la makusanyo ya maduhuli yaliyokusanywa na kuwasilishwa Hazina kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Februari 2023 hadi kufikia shilingi bilioni 457.23 ikilinganishwa na shilingi bilioni 412.09 kwa kipindi kama hicho mwaka 2021/22.

Amesema marekebisho ya sheria na kanuni zimewezesha kurasimisha shughuli za uchenjuaji wa madini na kuiwezesha Serikali kujua mashapo kupitia tafiti za GST na kufanya majadiliano yenye tija na kampuni za madini ambazo Serikali inashiriki katika ubia.

Awali, akitoa salam  katika mkutano huo Mwakilishi kutoka TUGHE Makao Makuu   Nsubisi Mwasandende amesema Chama kitaendelea kushirikiana na wizara na kueleza kuwa, TUGHE imeshuhudia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Sekta yaMadini

Naye, Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Wizara ya Madini Joseph Ngulumwa amesema  watumishi wizara ya madini wanajivunia uongozi wa wizara kutokana na namna unavyosimamia utekelezaji wa majukumu ya wizara na watumishi na kueleza kuwa, TUGHE wizarani itaendelea kushirikiana na wizara.

Akifunga mkutano huo, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesisitiza watumishi kushirikiana kwa karibu ikiwemo kubadilisha taarifa ambazo zitawezesha kutekelezwa kikamilifu kwa majukumu ya Wizara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post