TANZANIA NA INDIA KUENDELEZA UHUSIANO WA KIBIASHARA NA UWEKEZAJI


Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, akiongea na Balozi wa India nchini Mhe. Binaya Srikanta Pradhan na ujumbe wake Machi 27, 2023 katika Ofisi ndogo ya Wizara, jijini Dar es Salaam. Dkt Kijaji amewakaribisha wawekezaji wenye nia kutoka India kuja kuwekeza nchini katika viwanda vya dawa na vifaa tiba na viwanda vya kuongeza thamani mazao ya Parachichi na Mbaazi zinazohitajika kwa wingi katika soko la India.

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa India nchini Mhe. Binaya Srikanta Pradhan na ujumbe wake Machi 27, 2023 katika Ofisi ndogo ya Wizara, jijini Dar es Salaam. Dkt Kijaji amewakaribisha wawekezaji wenye nia kutoka India kuja kuwekeza nchini katika viwanda vya dawa na vifaa tiba na viwanda vya kuongeza thamani mazao ya Parachichi na Mbaazi zinazohitajika kwa wingi katika soko la India.


Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) na Balozi wa India nchini Mhe. Binaya Srikanta Pradhan wakipeana mikono baada ya mazungumzo ya kuhusu kuendeleza uhusiano wa kibiashara na uwekezaji baina ya Tanzania na India na Machi 27, 2023 katika Ofisi ndogo ya Wizara, jijini Dar es Salaam. India imetoa soko la Mbaazi tani 200000 kutoka Tanzania.

Na.Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM



Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) amewakaribisha wawekezaji wenye nia kutoka India kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali hususani viwanda vya kutengeneza dawa na vifaa tiba, uchumi wa bluu na viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo kama Parachichi na Mbaazi zinazohitajika kwa wingi katika soko la India.

Dkt. Kijaji ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo kuhusu kuendeleza uhusiano wa kibiashara na uwekezaji baina ya Tanzania na India na Balozi wa India nchini Mhe. Binaya Srikanta Pradhan Machi 27, 2023 katika Ofisi ndogo ya Wizara, jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kijaji amemhakikishia Balozi huyo kuwa Tanzania iko tayari kupokea wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya Anga, Utalii, kilimo na Afya hususan katika viwanda vya dawa na vifaa tiba ili kupunguza gharama za uagizaji dawa nje ya nchi.

Aidha, amemshukuru Balozi huyo wa India kwa upatikanaji wa soko la mbaazi za Tanzania tani 200000 nchini India na kushauri wawekezaji kitoka nchini himo kija kiwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani katika mazao ya kilimo ambayo husafirishwa zaidi katika nchi hiyo ikiwemo Mbaazi na Parachichi ili kuongeza ajira na pato la Taifa pamoja na kuhakikisha soko la mazao hayo linalotabirika.

Naye Balozi wa India nchini Tanzania Mhe. Binaya Srikanta Pradhan amesema India imekuwa na uhusiano mzuri wa Kibiashara na uwekezaji na Tanzania hususani katika viwanda vya uchakataji wa mazao ya kilimo, huduma za benki, madini na afya.

Aidha, Balozi huyo amesisitiza kuwa India itaendelea kushirikiana na kuendeleza uhusiano wa kibiashara na uwekezaji baina ya nchi hizo pamoja na kuwaunganisha wawekezaji wa Tanzania na India kufanya biashara pamoja kupitia makubaliana ya kibiashara yaliyopo na maonyesho mbalimbali yakiwemo maonyesho ya kimataifa ya biashara yanayojulikana kama sabasaba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments