MRADI KUZINGATIA HAKI ZA MAKUNDI MAALUM KATIKA UMILIKI WA ARDHI


Wataalam kutoka Benki ya Dunia pamoja na Wataalam wa Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) wakiangalia ramani ya mipango miji katika mtaa wa Mkwawa Kata ya Mpunguzi, Jijini Dodoma


Wataalam kutoka Benki ya Dunia pamoja na Wataalam wa Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) wakikagua maeneo ambayo shughuli za urasimishaji zinatekelezwa katika mtaa wa Bihawana Kata ya Mbabala, Jijini Dodoma


Wataalam kutoka Benki ya Dunia pamoja na Wataalam wa Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) wakikagua moja ya miundombinu ya upimaji iliyowezeshwa na mradi katika mtaa wa Bihawana Kata ya Mbabala, Jijini Dodoma

Na Magreth Lyimo WANMM

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi umedhamiria kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kwa wananchi kwa kuzingatia haki na usawa katika jamii.

Hayo yalisemwa na Mratibu wa Mradi Bw. Joseph Shewio wakati wa ziara ya viongozi kutoka Benki ya Dunia pamoja na Wataalam wa Mradi walipotembelea Mtaa wa Bihawana na Mtaa wa Mkwawa tarehe 29/03/2023 ili kushuhudia zoezi la urasimishaji linaloendelea katika mitaa hiyo Jijini Dodoma.

Bw. Shewio alisema ‘‘mradi umedhamiria kuhakikisha kuwa maeneo ambayo mradi utatekelezwa utazingatia taratibu zote na kanuni za upangaji, upimaji na umilikishaji pamoja na kusimamia haki na usawa katika jamii zetu’’.

‘‘Lengo la Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi pamoja na mengine mengi ni kutoa elimu ya umiliki kwa wanawake ili kuongeza umiliki wao ambao utawasaidia katika kukuza uchumi pamoja na kupunguza migogoro katika mirathi’’ alisema Bw. Shewio.

Mratibu wa Mradi huo alisisitiza kuwa mbali na kuongeza umiliki kwa wanawake mradi huu umejikita pia kuangalia haki ya umiliki ardhi wa makundi maalumu kama wazee, walemavu, Watoto, vijana, jamii za kifugaji na kiwindaji.

Nae Bi. Victoria Stanley ambae ni Mtaalamu kutoka Benki ya Dunia aliipongeza wizara kwa kupitia timu ya mradi kwa jitahada walizofanya hasa katika upande wa kuhakikisha kuwa wananchi wanashirikishwa katika kila hatua ya utekelezaji wa mradi.

Katika ziara hiyo Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Mhe. Prof. Davis Mwamfupe alishukuru timu ya mradi kwa kulichagua Jiji hilo kama sehemu ya kufanyia majaribio ya Mradi huo na kwamba jambo hilo ni fursa kwa wananchi kwani kilio na shauku ya wana Dodoma ni kuona maeneo yao yanapimwa na kumilikishwa kwa wananchi.

Diwani wa Kata ya Mbabala mtaa wa Bihawana Bi. Paskazia Mayala aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea mradi huo na pia kwa mtaa wao kuwa miongoni mwa mitaa ambayo mradi unatekelezwa na kuahidi ushirikiano katika kila hatua ya utekelezaji wa mradi huo.

Aidha alisema kuwa wananchi wa mtaa wa bihawana wamepata elimu ya kutosha kuhusiana na mradi ambayo itapelekea ongezeko la umiliki wa ardhi kwa wanawake na haki za makundi maalum zitalindwa.

Ziara hiyo ni mwendelezo wa ziara za kikazi za wataalam wa Benki ya Dunia katika kuangalia utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki za Ardhi unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa muda wa miaka mitano kuanzia mwaka 2022-2027 ukiwa na lengo la kuboresha usalama wa milki za ardhi nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments