BENKI YA CRDB YATWAA TUZO YA BENKI BORA KATIKA UTOAJI HUDUMA KWA WAJASIRIAMALI


Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Bonaventure Paul akipokea cheti cha Benki Bora inayohudumia wafanyabiashara wadogo na wakati nchini inayotolewa na Jarida maarufu la Global Finance kwa mwaka 2023, kutoka kwa Mwanzilishi na Mhariri Mtendaji wa Global Finance, Joseph Giarraputo (kulia) katika hafla ya kukabidhi tuzo iliyofanyika hivi karibuni jijini London, Uingereza
Na Mwandishi Wetu


BENKI ya CRDB imetwaa tuzo ya Benki Bora inayohudumia wafanyabiashara wadogo na wa kati Tanzania inayotolewa na Jarida maarufu la Global Finance kwa mwaka 2023. Hafla ya utoaji wa tuzo hizo ilifanyika hivi karibuni jijini London, Uingereza.

Jarida la Global Finance linawasaidia wakuu wa mashirika, benki na wawekezaji kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya biashara na fedha na viwango vya jarida hilo vimeaminika kwa benki na washirika.

Benki zilizopata tuzo hiyo kwa mwaka huu zimechaguliwa kutoka miongoni mwa benki nyingi ulimwenguni kutoka kwenye mabara ya Afrika, Asia-Pacific, nchi za Caribbean, Ulaya Mashariki na Kati, Amerika ya Kusini, Mashariki ya Kati, Amerika ya Kaskazini na Ulaya Magharibi.

"Ni heshimu kubwa kwetu kupokea tuzo hii maalum ambayo ni ushuhuda wa wazi kwenye mchango wetu kwa biashara ndogo na za kati nchini Tanzania.

"Utendaji wetu kwenye sekta hii umetokana na mpango mkakati na ushirikiano ambao umetuwezesha kuendelea kukuza uwezo wetu katika utoaji wa huduma za kifedha," alisema Bonaventure Paul, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo wa Benki ya CRDB.

Hivi karibuni, Benki ya CRDB ilipokea mkopo wa Euro milioni 150 kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) ambao utaongeza upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya biashara ndogo na za kati nchini, zikiwamo zinazomilikiwa na wanawake na kuwezesha uchumi wa bahari.

Mkopo wa EIB utasaidia kukuza biashara, kuleta usawa wa kijinsia na wanawezesha wanawake, pia kuziwezesha kampuni za uchumi wa bahari kuwekeza kwa maendeleo ya baadaye.


Benki ya CRDB imepewa tuzo hiyo kwa Tanzania kutokana na utafiti huru, ukihusisha wataalamu wa ndani ya sekta ya benki, viongozi waandamizi na wabobezi wa teknolojia kwa kutumia taaluma ya masoko na mahitaji, bidhaa na huduma, msimamo wa soko na ubunifu.

Tuzo hiyo inadhihirisha utayari wa Benki ya CRBD kuwezesha wateja wake kufanikiwa kwa kuhakikisha kwamba kila mmiliki wa kampuni ndogo na ya kati anapata usaidizi ili kufikia malengo yake ya mahitaji ya kibenki.

Tuzo za mwaka huu zimezingatia utendaji kwa kipindi cha kuanzia Aprili Mosi, 2021 hadi Machi 31, 2022.

Ni benki tano tu Afrika zimepewa tuzo hiyo, CRDB ikiwa ni benki pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments