GGML, STAMICO WASAINI MKATABA WA SH BILIONI 55.2 KUCHORONGA MIAMBA


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), Elder Damon (kushoto) akisaini mkataba kati ya kampuni hiyo na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) wenye thamani ya Sh bilioni 55.2 kwa lengo la kuendeleza shughuli za uchorongaji miamba kwenye migodi ya kampuni hiyo. Kulia na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk. Venance Mwasse.


Na Mwandishi wetu

KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), imesaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh bilioni 55.2 kwa lengo la kulipatia shirika hilo kandarasi ya kuchoronga miamba ndani ya mgodi wa GGML.


Akizungumza katika hafla fupi ya kutia saini makubaliano hayo jana mjini Geita, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Elder Damon alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa kanuni za ushirikishaji wazawa kwenye shughuli za uchimbaji madini mwaka 2018, idadi ya wafanyabiashara watanzania waliofanikiwa kushinda kandarasi mbalimbali ndani ya mgodi huo, imeongezeka.


"Nia yetu imekuwa kusaidia jamii kwa kuwapa ujuzi ili kuwawezesha kushindana kikamilifu. STAMICO imekuwa ikitoa huduma za uchorongaji miamba ndani ya GGML, kusaidia programu za uchimbaji wa wazi tangu Septemba 2020.


“STAMICO imetoa huduma za uchorongaji miamba kwa viwango vya juu kwa kuzingatia usalama na ufanisi katika sekta ya uchimbaji madini kulingana na malengo ya sekta hii. Makubaliano haya na STAMICO yanaonyesha uungaji mkono unaoendelea katika ukuzaji wa ujuzi na utaalamu kuhusu uchorongaji miamba na utafiti wa madini nchini,” alisema Damon.


Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk. Venance Mwasse aliipongeza GGML kwa imani waliyoionesha kwao tangu walipoanza kufanya kazi mwaka 2020.


“Tunapenda kuwahakikishia GGML na Serikali kuwa kazi yetu itatekelezwa kwa ubora na viwango vya juu,” alisema Dkt. Mwasse.

Mgeni rasmi aliyehudhuria hafla ya utiaji saini, Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko alisema kuwa hali ya STAMICO imebadilika na kuwa bora zaidi tangu mkataba wao wa awali na Geita Gold Mining Limited ulipoanza.


“Tangu 2020 STAMICO iliposaini mkataba wake wa kwanza na GGML, mambo yameboreshwa ndani ya Shirika. STAMICO imefanya vizuri sana kwa kuzingatia ubora na ufanisi wa kazi jambo ambalo wengi wetu tunajivunia.

“STAMICO imeiwakilisha vizuri nchi yetu ndiyo maana wawekezaji wengi kama GGML bado wana imani ya kufanya nao kazi,” alisema Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko alizitaka kampuni nyingine za ndani kunufaika na zabuni za nje kila zinapotangazwa kwa sababu kanuni za sheria hiyo ya madini ya mwaka 2017 zinatoa nafasi kwa watanzania kuchangamkia fursa zinazojitokeza kwenye sekta ya madini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments