BRELA YATOA UFADHILI KWA WANAFUNZI 5 WANAOSOMA ‘MASTERS’ YA MILIKI UBUNIFU

 

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi watano ambao wanasoma Shahada ya Uzamili katika fani ya Miliki Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


Akikabidhi hundi hizo za ufadhili leo Machi 10, 2023 Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amesema kuwa Wakala inafanya kila jitihada kuhakikisha watalaamu wanaongezeka na elimu ya Miliki Ubunifu inawafikia watu wengi zaidi.

Ameongeza kuwa kwa kushirikiana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamefanikisha kuwepo kwa mafunzo hayo ya Miliki Bunifu ambayo kwa kiasi kikubwa yataongeza uelewa na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Ndugu Waandishi wa Habari tumetoa ufadhili huu kwa kuzingatia jinsia na makundi maalum na kwa awamu hii tumefadhili wanafunzi watano na kiasi cha Shilingi Milioni Kumi na Sita Laki Tano na Elfu Hamsini (16,550,000/=) Kimetolewa”, amesema Bw. Nyaisa.

Amewataja wanafunzi hao waliopata ufadhili kuwa ni pamoja na Bi. Grace Ezekiel Mwaikono kutoka Mahakama Kuu, Bw. Stanslaus Aidan Kigosi kutoka BRELA, Bw. Addo November Mwasongwe kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Eric Maximillian Mlasani kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Bi. Merciana Nehemiah Ntabaye kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Vilevile, ametaja lengo la ufadhili kwa wanafunzi hao kuwa ni kupanua wigo wa utaalamu katika nyanja ya Miliki Ubunifu kwakuwa eneo hilo muhimu halina wataalamu wengi hapa nchini, kuongeza ufahamu kuhusu Miliki Ubunifu kwa maendeleo chanya ya Taifa la Tanzania kutokana na umuhimu wake katika maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.

Ameongeza kuwa ufadhili huo utahamasisha wanufaika kutambua faida zinazopatikana kutokana na elimu kuhusu Miliki Ubunifu na jinsi ya kuitumia katika kuendeleza na kukuza Ubunifu nchini, kuweka mkazo mahsusi katika muunganisho wa sheria na sera za Miliki Ubunifu katika muktadha wa mienendo iliyopo ya kiuchumi na kijamii inayopatikana barani Afrika.

Kwa upande wake Dkt. Sosthenes Materu, ambaye ni Amidi wa Shule Kuu ya Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amewashukuru BRELA kwa ufadhili huo sambamba na jitihada za Taasisi hiyo katika kuendeleza Miliki Ubunifu kwa ajili ya kuchochea maendeleo.

Mwailishi wa wanufaika wa ufadhili wa BRELA ambaye ametoka katika kundi la watu wenye mahitaji maalumu Bw. Erick Maximillian Mlasani, ameishukuru BRELA kwa ufadhili huo na kuahidi baada ya kuhitimu watakuwa miongoni mwa wataalamu watakaojitoa kwa jamii ili elimu ya Miliki Ubunifu ifike mbali zaidi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post