WIZARA YA ELIMU YAELEZA MSIMAMO WAKE SAKATA LA NECTA KUACHA KUPANGA SHULE NA WANAFUNZI BORA

 

Waziri wa elimu,Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda.

Na Dotto Kwilasa, DODOMA

KUFUATIA kuwepo kwa hoja ya Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA)  kutotangaza shule na wanafunzi bora kwamba kunadhoofisha elimu, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema 
utaratibu huo ulikuwa ukilaumiwa na wataalam wa elimu. 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameelezea msimamo juu ya NECTA wa kutotangaza shule na wanafunzi bora kuwa NECTA imeacha kupanga shule kwa ubora kutoka na sababu ya utata wa jambo hilo.

Hatua hiyo ni kufuatia mwongozo ulioombwa na  Mbunge wa Bunda Vijijini (CCM), Mwita Getere kudai kumekuwa na minong’ono kuwa kutotangazwa kwa mpangilio wa ufaulu kunadhoofisha elimu ya Tanzania.


Mbunge huyo amehoji ,"Kwa kuwa Serikali imo humu ndani kwanini isitoe taarifa humu ndani kipi bora, hayo matangazo waliyositisha yana umuhimu gani kwa wananchi na yana ubora gani kwa wananchi,” 


Akijibu mwongozo huo leo Bungeni  Profesa Mkenda amesema,"Chukua shule ambayo ina watoto 100, nyingine ina wanafunzi 20, wamemaliza kidato cha nne, wanafunzi 170 wapata alama A, 30 hawakupata A, wenye wanafunzi 20 wote wamepata A kwa kuangalia wastani ufaulu ni wazi wenye wanafunzi 20 itatangazwa ni shule bora.


“Wengine watasema shule ya wanafunzi 70 wakapata A si bora zaidi, kuliko shule ya wanafunzi 20 tu. Ukiacha aina hiyo ya tathimini inaweka shinikizo kwa shule ya wanafunzi 100 kwa mfano kuhakikisha inawaondoa wale 30 waweze kutangazwa shule bora”, amesema.


Prof.Mkenda ameema , kuna njia tatu zinaweza kutumika kufanya tathmini ikiwa ni pamoja na kuangalia matokeo ya mwisho ya mitihani kama iliyokuwa ikifanywa na NECTA na kwamba tatizo la njia hiyo haisemi shule imechangia nini katika maendeleo ya mtoto husika.


"Njia hiyo imeacha kutumiwa na nchi nyingi duniani na badala yake wanatumia nyongeza ya thamani (value edition) kwa kuangalia mwanafunzi alianza akiwa vipi na shule imechangia nini katika kumwinua mtoto katika masomo yake," amefafanua.


"Kwa maana hiyo shule bora inaweza kuwa ya kata tu, imechukua wanafunzi wanaoonekana wa wastani lakini wanapomaliza ile shule ikawa na matokeo mazuri kwa kuongeza ubora wa wanafunzi kuliko ile inayochagua wanafunzi bora tu,”amesema.


Kuhusu  njia ya tatu amefafanua  kuwa si kwamba inaangalia mtoto aliingiaje shuleni bali na mazingira yake yakoje na kutolea mfano shule iko katika mzingira magumu maji hayapatikani karibu, hakuna mabweni na jamii masikini.


"Njia hiyo inaangalia japo mazingira hayo magumu lakini walimu wakafanya kazi na kuhakikisha mwanafunzi aliyeingia kwa wastani anapata daraja A,katika mazingira hayo, shule hiyo itakuwa imeongeza kikubwa kuliko mwenye historia ya kuchukua wanafunzi mwenye ufaulu wa juu na katika mitihani yake ya mwisho akapata ufaulu mkubwa," amesema.


Amesema tathimini hiyo inahitaji wataalam wa takwimu na kwamba watakapokuwa na tathimini hiyo ndio wanaweza kuwaambia wazazi kuwa shule ipi ni bora.


Amesema  hawajazuia mtu yoyote kusema shule ipi ni bora na kwamba matokeo yapo katika mtandao na Serikali haijaficha hilo na kusisitiza kuwa baraza halichukui kutangaza matokeo ambayo kisayansi yamelaumiwa na wataalam wa elimu. 


Hata hivyo amesema  huko mbele baraza litaangalia namna nzuri ya kupangilia mambo hayo yote na kwamba Wizara haiwezi kuondoa  ushindani na ndio maana imeweka madaraja.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments