KATAMBI AFAFANUA MADAI YA WALIOKUWA WAFANYAKAZI WA KILTEX NA SUNGURATEX


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi,akijibu Swali
la msingi la Mbunge wa Ukonga, Mhe.Jerry Silaa.
Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji lini Serikali itawalipa mafao waliokuwa wafanyakazi wa viwanda vya Kiltex na Sunguratex Gongolamboto.

................................

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, amesema kuanzia mwaka 1989 Serikali kupitia Mifuko ya NSSF na uliokuwa PPF iliwalipa mafao waliokuwa wafanyakazi wa viwanda vya Kiltex na Sunguratex Gongolamboto baada ya ukomo wa ajira zao.

Mhe.Katambi ameyasema hayo leo Februari 1, 2023 bungeni alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Ukonga, Mhe.Jerry Silaa.

Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji lini Serikali itawalipa mafao waliokuwa wafanyakazi wa viwanda vya Kiltex na Sunguratex Gongolamboto.

Akijibu swali hilo, Mhe.Katambi amesema mwezi Aprili 2022 Mfuko wa PSSSF ulipokea malalamiko ya waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda Sunguratex wapatao 644 wakidai kuwa hawakulipwa mafao yao kikamilifu na uliokuwa Mfuko wa PPF.

“Baada ya Mfuko kufanya uchambuzi wa madai hayo, imeonekana kuwa wafanyakazi hao walishalipwa mafao kikamilifu isipokuwa baadhi yao wanasubiri kufikisha miaka 55 ili waanze kulipwa pensheni ya mwezi,”.

Hata hivyo, amesema mfuko haujapokea malalamiko yoyote kuhusu wafanyakazi wa kiwanda cha Kiltex.

“Serikali ipo tayari kuendelea kushirikiana na Mhe. Mbunge kutatua changamoto za waliokuwa wafanyakazi wa viwanda vya Kiltex na Sunguratex Gongolamboto,”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post