TBA KUTEKELEZA MIRADI YA UJENZI NYUMBA 3500 ZA WATUMISHI WA UMMA




Na Dotto Kwilasa, Malunde I Blog,DODOMA.

SERIKALI imetoa jumla ya shilingi bilioni 54.2 kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba 3500 za watumishi wa umma katika eneo la Nzuguni Dodoma ambapo mradi huo uliwekwa jiwe la msingi na Makamu wa Rais  Dk. Philip Mpango Novemba 30 mwaka jana.

Hayo yamebainishwa jijini hapa na Mtendaji Mkuu wa TBA Daud Kondoro wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu wa wakala huo katika kipindi cha miaka miwili.

Licha ya hayo amesema Serikali itaendelea kuiwezesha TBA kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa ikiwa ni Pamoja na kutoa fedha za ruzuku kwa ajili ya kutekeleza miradi  ya serikali. katika kipindi cha miezi 18 na kwamba tayari imetoa  sh. bilioni 54.2 kwa  ajili ya utekelezaji wa miradi.

Amefafanua kuwa serikali imeshatoa sh.bilioni 15.5 kwa kuanza utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba 150 ambao umefikia asilimia 81 na awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 150 za awamu ya pili ukiwa umefikia asilimia tatu.

“Mradi wa ujenzi wa nyumba 20 za viongozi jijini Dodoma ambao umegharimu sh.bilioni tisa mradi huu ulitekelezwa ili kukabiliana na uhaba wa nyumba za makazi ya viongozi uliojitokeza mara baada ya serikali kuhamishia makao yake makuu jijini Dodoma  mradi huu umeshakamilika kwa asilimia  100,”amesema.

Ametaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma katika eneo la magomeni kota, awamu ya kwanza na ya pili ambao unagharimu sh.bilioni  7.8 ambapo  ujenzi wa jengo la ghorofa nane lenye uwezo wa kuchukua familia 16 tayari limeshakamilika kwa asilimia 99.

Amebainisha kuwa katika  ujenzi wa awamu ya pili  jengo la ghorofa nane  umefikia asilimia  25 huku mradi mwingine wa nyumba za makazi ya watumishi wa umma katika eneo la Temeke Kota ukiendelea ambapo linajengwa jengo la ghorofa tisa   linalochukua familia 144.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments