WANANCHI DUGUSHILU WATEMA NYONGO MBELE YA DC MKUDE.... "HAKUNA MIUNDOMBINU, TUMEDANGANYWA SANA"

Wakazi wa kijiji cha Dugushilu kata ya Igaga wilayani Kishapu wakiwa kwenye mkutano wa hadhara

Mkuu wa wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude akizungumza na wananchi wwa kijiji cha Dugushilu kata ya Igaga wilayani Kishapu

Na Sumai Salum - Kishapu

Wananchi wa kijiji cha Dugushilu kata ya Igaga wilayani Kishapu wamemuomba mkuu wa wilaya hiyo , Joseph  Mkude kuwasaidia  kutatua kero zao kwa haraka kwani zimesababisha kuchelewa kwa maendeleo kijijini hapo.


Wametoa ombi hilo Jana Februari 20, 2023 kwenye mkutano wa hadhara wa kuzungumza masuala ya maendeleo ya kijiji na Kata ambapo wamesema kuwa kumekuwa na ahadi zisizotekelezeka kwa viongozi mbalimbali waliopita hapo kuhusu utatuzi wa changamoto ya miundombinu ya barabara,zahanati ya kijiji,umeme pamoja na maji.

Mkazi wa kijiji hicho, Agnes Ng'ombeyapili amesema kuwa ujio wa mkuu wa wilaya  unawapa imani kuwa atafuatilia utatuzi wa changamoto ya ukosefu wa maji na umeme kiasi ambapo ukosefu wa maji kuhatarisha uhai wao na afya ya ndoa.


 "Mkuu wetu wa wilaya tunamashukuru umefika hapa ujue wagombea wakija wamekuwa wakitoa ahadi bila kutekeleza tunaambiwa tutaletewa umeme tunapiga vigeregere,tunawatandikia hadi vitenge vyetu chini wanavikanyaga lakini hamna kitu na kuhusu swala la ukosefu wa maji tunaamka saa 10 usiku na fisi ni wengi lakini kwa kuwa hatuna visima vya kudumu hatuna namna zaidi ya kukabiliana nao kwa kujificha ili tupate maji", amesema Agnes.


Aidha wakati akichangia hoja ya miundombinu ya barabara Bw. Julius Joseph amesema kuwa Dugushilu wamefanywa  kijiji cha kuchukulia Kura kwa sababu kwa muda mrefu wanaambiwa kuletewa barabara hadi leo hakuna barabara ya kuelekea makao makuu ya wilaya(Mhunze) hakuna barabara la uhakika  kuelekea Ukenyenge na hata Uchunga.


"Kuna jengo la zahanati tuliambiwa tujenge na serikali itamalizia mpaka sasa hakuna kilichofanyika zaidi limegeuzwa kuwa jumba la taka sasa kama na wewe umekuja kuzungumza tu na usifanye utekelezaji sawa hatuna jinsi lakini bado tunaimani na wewe utatekeleza", ameongeza Joseph.


Naye Ndunguli Salula  mbali na kumpomgeza Mkude  kuwa  DC wa kwanza kufika kwenye mkutano wa hadhara kijijini hapo, amesema kuwa wamechoshwa na propoganda za wanasiasa kuwaahidi kuwaletea maendeleo na baadae wakiwauliza sababu ya kucheleweshwa wanasema serikali itafanya baadae hivyo ni bora wanasema ukweli mapema ili wawe huru.

 

Hata hivyo Diwani wa Kata hiyo ya Igaga Mhe. James Kamiga alimaarufu BONYA'S amesema, amekuwa akisumbua ofisi za Tarura,Tanesco,Mipango na ofsi ya Maji na wameahidi utekelezaji kufanyiwa haraka ambapo tayari wamepokea Shilingi milion 50 kutoka ofisi ya mipango ili kumalizia  jengo la zahanati na mahali ambapo hapajakamilika wananchi watajitahidi kukamilisha kwa sababu ni huduma muhimu kwao hivyo wakati wa utekelezaji miradi hiyo ya kimikakati mwananchi yoyote asizuie shughuli za utekelezaji.


Kwa upande wake Mkuu wa wilaya Kishapu, Joseph Mkude amewahakikishia wananchi wa Dugushilu  kuwa serikali ya awamu ya sita inawahakikishia kuwasogezea huduma kwa kushirikina na wananchi hivyo wawe na utayari kutoa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa shule ili kupunguza changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu na watambue kuwa hakutakuwa na fidia iwapo nguzo za umeme,Bomba za maji na huduma zingine za jamii zikipita kwenye maeneo yao.

 

Sambamba na hayo Mkude amechangia kiasi ya shilingi laki nne 400,000 kwa ajili ya ukamilishaji boma la zahanati ya kijiji pamoja na ujenzi wa shule ya msingi kijijini hapo.Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments